Michezo

Ibrahimovic afunga mawili na kusaidia AC Milan kuzamisha Bologna katika Serie A

September 23rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI mkongwe Zlatan Ibrahimovic alifunga mabao mawili na kusaidia AC Milan kuanza vyema kampeni za Serie A baada ya kuipepeta Bologna 2-0 uwanjani San Siro mnamo Septemba 21, 2020.

Ibrahimovic, 38, alikamilishwa kwa kichwa krosi safi aliyopokezwa na Theo Hernandez katika dakika ya 35 kabla ya kufunga la pili kupitia penalti mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Awali, Ibrahimovic alikuwa amepoteza nafasi kadhaa za wazi huku mojawapo ya makombora yake yakigongwa mwamba wa goli la Bologna.

Ibrahimovic kwa sasa amefunga mabao mawili katika mechi tatu kati ya tano zilizopita za Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Mchuano dhidi ya Bologna ulikuwa wa kwanza kwa fowadi wa zamani wa Manchester City, Brahim Diaz kuchezea Milan tangu asajiliwe kutoka Real Madrid kwa mkopo. Aidha, huu ni msimu wa nne mfululizo ambapo Ibrahimovic amefunga bao katika mechi ya ufunguzi wa msimu wa Serie A.

Kipa wa Milan, Gianluigi Donnarumma alifanya kazi ya ziada kunyima wavamizi wa Bologna nafasi nyingi za ziada. Hata hivyo, Bologna walikamilisha mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Mitchell Dijks kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la pili katika dakika ya 88.

Chini ya kocha Stefano Pioli, Milan walikamilisha kampeni za msimu uliopita katika nafasi ya sita kwa alama 17 nyuma ya mabingwa mara tisa mfululizo, Juventus. Milan kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Crotone ugenini katika mechi ijayo ya Serie A mnamo Septemba 26, 2020.