Michezo

Ibrahimovic afunga mawili na kusaidia AC Milan kuzamisha chombo cha Napoli katika Serie A

November 23rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ZLATAN Ibrahimovic aliendeleza ubabe wake katika ulingo wa soka kwa kufunga mabao mawili yaliyosaidia waajiri wake AC Milan kupepeta Napoli 3-1 na kuendeleza rekodi ya kutoshindwa kwa miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) hadi kufikia sasa msimu huu.

Fowadi huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 39 sasa anajivunia jumla ya mabao 10 kutokana na mechi sita zilizopita za Serie A.

Hata hivyo, alipata jeraha la paja lililomlazimisha kuondoka uwanjani akichechemea katika kipindi cha pili.

Ibrahimovic ambaye ni raia wa Uswidi, aliwafungulia Milan ukurasa wa mabao kunako dakika ya 20 baada ya kukamilisha kwa kichwa krosi aliyopokezwa na Ante Rebic.

Baada ya Ibrahimovic kufungia waajiri wake bao la pili katika dakika ya 54, Dries Mertens alisawazishia Napoli katika dakika ya 63, sekunde chache kabla ya kiungo Tiemoue Bakayoko anayechezea Napoli kwa mkopo kutoka Chelsea kuonyeshwa kadi nyekundu.

Jens Petter Hauge ambaye ni raia wa Norway, alikamilisha karamu ya ufungaji wa mabao kwa upande wa AC Milan mwishoni mwa kipindi cha pili na kuhakikisha kwamba wanatia kapuni alama zote tatu zilizowapaisha hadi kileleni mwa jedwali la Serie A.

Milan kwa sasa wanajivunia pointi 20, mbili zaidi kuliko Sassuolo wanaokamata nafasi ya pili. AS Roma wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 17, moja mbele ya mabingwa watetezi Juventus wanaofunga mduara wa nne-bora.