Ibrahimovic atambisha Uswidi katika mechi ya kwanza tangu abatilishe maamuzi ya kustaafu soka ya kimataifa

Ibrahimovic atambisha Uswidi katika mechi ya kwanza tangu abatilishe maamuzi ya kustaafu soka ya kimataifa

Na MASHIRIKA

ZLATAN Ibrahimovic alichangia bao katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Uswidi dhidi ya Georgia katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Ibrahimovic anayechezea AC Milan ya Italia kusakatia Uswidi tangu atangaze kurejea kutandaza soka ya kimataifa licha ya kustaafu miaka mitano iliyopita.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 39 alitoa krosi safi iliyojazwa kimiani na Viktor Claesson katika dakika ya 35.

Georgia walikuwa na fursa chache za kufunga mabao katika mchuano huo ila mshambuliaji Levan Shengelia alishuhudia fataki yake ikipanguliwa na kipa Kristoffer Nordfeldt mwishoni mwa kipindi cha pili.

Marejeo ya Ibrahimovic katika timu ya taifa yamaanisha kwamba ndiye kwa sasa mchezaji mkongwe zaidi kuwahi kuchezea kikosi cha Uswidi.

Nyota huyo amevunja rekodi ya awali ya kipa Thomas Ravelli aliyewahi kuchezea Uswidi akiwa na umri wa miaka 38 na siku 59.

Ibrahimovic ambaye kwa sasa anajivunia mabao 62 kutokana na mechi za kimataifa, nusura afunge goli mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya kuondolewa uwanjani katika dakika ya 84.

“Nilihisi kana kwamba hiyo ilikuwa mechi yangu ya kwanza kabisa ndani ya jezi za timu ya taifa. Nahisi kwamba nilikuwa na fursa ya kufanya mambo mengi mazuri zaidi uwanjani. Pengine nilishtuka, pengine matarajio yalikuwa mengi zaidi. Lakini muhimu zaidi ni kwamba tulishinda mchuano huo,” akasema Ibrahimovic katika mahojiano yake na Sverige Radio.

Ibrahimovic ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Uswidi, alifungia nchi yake jumla ya mabao 62 kutokana na mechi 116 kabla ya kustaafu mnamo 2016 baada ya Uswidi kubanduliwa kwenye fainali za Euro 2016 katika hatua ya makundi.

Alifichua azma ya kurejea katika timu ya taifa kupitia mahojiano aliyofanyiwa na mojawapo ya magazeti mnamo Novemba 2020. Baada ya kuweka wazi azma yake hiyo, kocha Janne Andersson alitua jijini Milan kukutana moja kwa moja na Ibrahimovic.

Kufikia sasa, Ibrahimovic amefungia AC Milan jumla ya mabao 14 kutokana na mechi 14 za Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Dkt Ruto akiungana na Raila, kipi kitarajiwe Mlima Kenya...

Gambia, Comoros, Gabon na Ghana kati ya mataifa saba zaidi...