Michezo

Icardi kujaza pengo la Diego Costa Atletico

April 19th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Diego Simeone wa Atletico Madrid ameanzisha mazungumzo na Wanda Nara ambaye ni mke na wakala wa mwanasoka Mauro Icardi kwa nia ya kufanikisha uhamisho wa mvamizi huyo mzawa wa Argentina.

Kwa mujibu wa Simeone, Icardi, 27, atakuwa kizibo kamili cha fowadi Diego Costa ambaye ataagana na Atletico mwishoni mwa msimu ujao.

Icardi ambaye amekuwa Paris Saint-Germain (PSG) kwa mkopo kutoka Inter Milan, amejivunia msimu wa kuridhisha hadi kufikia sasa ambapo amepachika wavuni jumla ya mabao 20 kutokana na mechi 31.

Ilivyo, PSG tayari wamekatiza uhusiano wao na Icardi kutokana na kauli za kutatanisha za mara kwa mara za Nara ambaye pia alikuwa kiini cha kusambaratika kwa uhusiano kati ya Icardi na Inter Milan, Italia.

Kukataliwa kwa Icardi kambini mwa Inter na PSG kunamfanya kivutio cha Atletico ambao wamekuwa wakiwania huduma za mshambuliaji atakayeshirikiana vilivyo na nyota wa zamani wa Chelsea, Alvaro Morata na chipukizi Joao Felix ambaye hajatamba jinsi ilivyotarajiwa uwanjani Wanda Metropolitano.

Iwapo Atletico wataambulia pakavu katika juhudi za kumshawishi Icardi kujiunga nao, kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) huenda kikaanza kuhemea huduma za mkongwe Edinson Cavani atakayebanduka katika kikosi cha PSG mwishoni mwa msimu huu.

Hadi kusitishwa kwa kampeni za La Liga kutokana na virusi vya corona, Atletico walikuwa katika nafasi ya sita jedwalini baada ya kujizolea jumla ya alama 45, moja nyuma ya Getafe na Real Sociedad wanaofunga mduara wa nne-bora. Sevilla wanashikilia nafasi ya tatu nyuma ya Real Madrid na viongozi Barcelona.