Makala

Idadi kubwa ya watu wasio na makao nchini Kenya ni wanaume, Ripoti mpya yasema

Na MARY WANGARI July 11th, 2024 2 min read

WANAUME wanaongoza kwa idadi ya watu wasio na makao nchini, inasema ripoti mpya.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Baraza la Kitaifa kuhusu Idadi ya Watu (NCPD) zaidi ya nusu ya wanaume wote nchini hawana makazi.

Wanaume wanane kwa kila 10 nchini hawana pahala wanapoweza kuita nyumbani hivyo kulazimika kuishi mitaani, jinsi inavyoashiriwa na Nakala ya Msimu Nambari Moja 2023, katika Sera ya Kitaifa kuhusu Idadi ya Watu Nchini.

Kulingana na Toleo la Tano la Nakala hiyo, wanaume wanajumuisha asilimia 80 ya watu wasio na makao kote nchini ambamo kwa jumla, kwa kila kundi la wanajamii 100,000 watu 42 hawana makao.

Kufuatia takwimu hizo, idadi kubwa ya wanaume nchini wameorodheshwa miongoni mwa makundi ya wanajamii walio hatarini yanayojumuisha watu wasio na makao, walemavu, mayatima na watu wenye viungo vyote viwili vya uzazi (huntha).

“Hali ya kukosa makao aghalabu huchukuliwa kuwa ishara na kiini cha ufukara na kutengwa kijamii. Masuala makuu yanayoathiri kitengo hiki cha wanajamii yanajumuisha kukosa makazi, umaskini, afya, elimu na kujumishwa kijamii,” alifafanua Mkurugenzi wa NCPD, Mohamed Sheikh.

Kuhusu kukosa makazi, wanaume (asilimia 80) wanafuatiwa na watoto wenye umri wa miaka mitano wasio na habari kuhusu walipo wazazi wao wanaojumuisha asilimia 56.

Akizungumza katika hafla ya kuzindua ripoti hiyo jijini Nairobi, Mkurugenzi wa NCPD alihimiza serikali “kusaka mikakati kabambe ya kuwezesha watu wasio na makao kupata makazi.”

Ripoti hiyo inayochapishwa kila baada ya miaka 10 imeorodhesha kuzorota kiafya, ukosefu wa usalama na kukosa huduma muhimu za kijamii kama masuala nyeti kisera yanayowakabili wanajamii wasio na makao nchini.

Idadi ya watu wasio na makao nchini imeongezeka karibu maradufu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Sensa iliyofanywa 2019 kuhusu Idad ya Watu na Makazi Nchini ilihesabu wanajamii 20,101 wasio na makao idadi ambayo ni chini ya asilimia moja ya jumla ya watu nchini.

Kwa sasa, jumla ya Wakenya 46,639 wanaishi mitaani huku Kaunti ya Nairobi ikiongoza kwa idadi ya watu 15, 337, wasio na mahala popote pa kuita nyumbani.

Kaunti nyinginezo zenye idadi kubwa ya watu wasio na makao, kulingana na ripoti hiyo ni pamoja na Mombasa  (7529), Kisumu (2746), Uasin Gishu (2147) na Nakuru (2005).

“Kitengo hiki cha wanajamii kinapatikana katika makundi yote ya wanajamii,” inaeleza ripoti hiyo.

“Kukosa kujiweza kunatokana na uyatima, ulemavu, au kushindwa kufanya shughuli za kila siku, ubaguzi katika jamii unaohusishwa na huntha na kukosa makao kutokana na kufurushwa au ufukara.”

Kenya kwa sasa imeorodheshwa kama Nchi yenye Mapato ya Chini kwa Wastan na nchi ya tisa kubwa zaidi kiuchumi katika bara la Afrika.

Hata hivyo, asilimia 18 ya Wakenya wanaandamwa na uchochole huku wakiishi kwa Sh255 kwa siku, jinsi inavyoashiriwa katika ripoti ya Benki ya Dunia 2022.