Makala

'Idadi ya samaki Ziwa Baringo imepungua kwa kiwango cha kutisha'

July 25th, 2019 2 min read

Na MAGDALENE WANJA

ASILIMIA kubwa ya mito inayotiririka kwenye Ziwa Baringo tayari imeanza kukauka.

Hii ni kutokana na kuchelewa kwa mvua, mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za binadamu miongoni mwa sababu zingine.

Hii imeathitri sana jamii ambazo zinaishi katika eneo la kisiwa cha Kokwa ikizingatiwa kwamba wengi wanategemea samaki kutoka ziwa Baringo kama njia ya kujihakikishia kipato na pia kama chakula.

Mvuvi aonyesha samaki wadogo kutoka Ziwa Baringo. Picha/ Magdalene Wanja

Yapo malalamiko kwamba samaki asilia wamepungua kwa sababu kuna aina ya samaki mla samaki aliyewekwa kwenye ziwa hilo na watafiti.

Kulingana na mtafiti wa Taasisi ya Utafiti kuhusu Viumbe wa Majini na Samaki, Kenya Marine and Fisheries Research Institute (KMFRI), Bw Cyprian Odoli (PhD), idadi ya samaki katika Ziwa Baringo imepungua kwa asilimia 50.

“Katika miaka ya 1960, Ziwa Baringo lilikuwa likitoa kati ya tani 500 na 600 za samaki ambapo wengi walikuwa ni aina ya ngege au Tilapia.

Ziwa Baringo lina aina nne za samaki ambazo ni pamoja na Lungfish, Catfish, Barbus, na Tilapia.

Samaki aina ya Tilapia walikuwa wengi miaka ya sabini (1970s) lakini idadi ikaanza kupungua mara tu baada ya samaki aina ya marbled lungfish kuletwa ziwani humo na watafiti.

Bw Odoli anasema kuwa aina hiyo ya samaki- lungfish – ndio ya kiwango cha juu zaidi ziwani humo kwa sasa.

“Kufikia sasa, idadi ya samaki imepungua hadi kiwango cha kati ya tani 100 na 300 kila mwaka,” anasema Odoli.

Bi Judy Loweri anayefanya kazi ya kutayarisha samaki katika eneo hilo anasema kupungua kwa samaki katika ziwa hilo kumetishia kusambaratisha kabisa kipato chao.

“Zamani biashara ya samaki ilivuma sana na wateja wengi walikuwa wakitoka miji kama Eldoret, Nakuru, Kabarnet na Marigat,” anasema Judy.

Naye Bw Jamleck Lenapunya ambaye ni mvuvi na mkazi wa eneo hilo anasema kiwango hicho kilipungua zaidi mnamo mwaka 2015.

Hata hivyo serikali ya Kaunti ya Baringo imeanzisha mpango wa kuweka mipaka kwenye ziwa hilo kama mojawapo ya njia za kuwapa nafasi samaki wadogo kukua.

Baadhi ya mito inayotiririka kwenye ziwa hilo ni pamoja na Endao, Makutan, Ol Araban ambayo ni ya msimu.

Mwanamke akiwa ameshika samaki mkubwa aliyevuliwa kutoka kwa Ziwa Baringo. Picha/ Magdalene Wanja