Habari za Kitaifa

Idadi ya waliofariki katika mkasa wa bwawa Maai-Mahiu yafikia 40

April 29th, 2024 1 min read

UPDATE: Taarifa kufikia 1pm zinasema idadi imepanda hadi watu 45

NA MERCY KOSKEI

IDADI ya waliofariki katika mkasa wa Jumatatu asubuhi wa bwawa mjini Maai-Mahiu imefikia 40.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nakuru Samuel Ndanyi amethibitisha kwamba kufikia saa sita mchana, takriban miili 40 ilikuwa imeopolewa kutoka kwa nyumba zilizoathirika.

“Tumepata miili 40 ambayo ilikuwa imezikwa kwenye matope. Tunashuku kwamba walikuwa wanajaribu kutoroka kutoka kwa tope lililogubika mtaa huo. Wengi wao walikuwa wanawake na watoto ambao hawangeweza kukimbia upesi, na pia wakongwe,” akasema Bw Ndanyi.

Wakati wa kisa hicho cha Jumatatu saa kumi asubuhi, maji yaliyokuwa yanapita kwa kasi yalifagia kila kitu njiani.

Magari yalisombwa na kugonganishwa kwenye majumba ambayo pia yalivurugwa hadi kwenye msingi.

Idara ya Afya ya Kaunti ya Nakuru imeanzisha juhudi za kupeleka msaada kwa waathiriwa kufuatia mkasa huo wa kutisha.

Mkurugenzi wa Mipango na Usimamizi Dkt Joy Mugambi anasema kitengo hicho kimetuma ambulansi iliyo na vifaa vya kushughulikia wagonjwa mahututi kusaidia katika shughuli za uokoaji.

Anasema ambulansi hizo na kikosi cha kukabiliana na majanga kimezuru maeneo ya mafuriko na kuokoa zaidi ya wahanga 42 walio na majeraha madogo na kuwapeleka katika hospitali za Maai-Mahiu na Naivasha.