Habari Mseto

Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko yafika 194

May 6th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

KWA muda wa saa 24 zilizopita watu 30 wamepoteza maisha yao kutokana na mafuriko.

Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa amesema Jumatano idadi jumla ya waliofariki kutokana na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali nchini imefikia 194.

Bw Wamalwa alitaja maeneo ya Garissa, Tana River, Nyando na Trans Nzoia kama yaliyoathirika pakubwa.

“Tafadhali, iwapo unaishi kando ya mito hamia sehemu ambazo ni salama. Mvua inaendelea kushuhudiwa, mito inafurika na kufuja kingo zake. Tafadhali, watu wasipuuze ilani zinazotolewa,” akaonya waziri Wamalwa.

Akitoa mfano wa Mto Tana, Nyando na Trans Nzoia, alisema waathiriwa wataendelea kuhamishiwa shuleni na ambapo serikali itawasaidia wakiwa humo.

“Serikali itaendelea kutoa misaada. Wizara ya maji inapelekea waathiriwa maji,” akaeleza.

Huku maambukizi ya Covid-19 yakiendelea kuongezeka nchini, Waziri Eugene amehimiza wizara ya afya kusambazia waathiriwa wa mafuriko maski ili kuzuia kuambikizwa virusi vya corona.

Wakati huo huo, Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali Dkt Fred Matiang’i amesema watakaokataa kuhama kwa hiari maeneo hatari, serikali haina budi ila kutumia nguvu kuwaondoa.

“Ni heri tutumie malori kuwaondoa ili kunusuru maisha ya watu. Tutakuja kujadiliana baadaye,” Dkt Matiang’i akasema, huku akiahidi serikali kuendelea kutoa misaada ya chakula na mahitaji ya kimsingi kwa waathiriwa.

Mvua ya mafuriko inaendelea kushuhudiwa maeneo tofauti nchini, maelfu wakiachwa bila makao baada ya nyumba zao kusombwa na maji.