Kimataifa

Idadi ya waliokufa kwenye ghasia Uganda yagonga 49

November 22nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KAMPALA, Uganda

IDADI ya watu waliofariki katika ghasia zilizozuka nchini Uganda Jumatano kwenye makabiliano kati ya wafuasi wa mgombea urais wa upinzani Robert Kyangulanyi na polisi imepanda hadi 49.

Kulingana na rekodi katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Mulago, miili ya watu 37 ililetwa katika hifadhi hiyo kutoka hospitali mbalimbali, ilhali wagonjwa 12 walifariki kutokana na majeraha hospitalini humo Jumatano na Alhamisi.

Msimamizi wa hospitali ya Mulago, David Niwamanya alisema baadhi ya wagonjwa walifariki dakika chache baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo ilhali wengine walifariki wakifanyiwa upasuaji kuondoa risasi miilini mwao.

Bw Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, alikamatwa Jumatano baada ya makabiliano kuzuka kati ya wafuasi wake na maafisa wa polisi waliokuwa wakivunja mkutano wa kampeni wa mwanasiasa huyo kwa misingi ya kukiuka msharti ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Zaidi ya watu 130 walijeruhiwa katika machafuko hayo.

Kukamatwa kwa mgombeaji huyo wa urais kulichochea maandamano jijini Kampala na miji mingi nchini Uganda.

Rais Yoweri Museveni alilaani machafuko hayo akisema, wafuasi wa upinzani ndio wanavuruga amani nchini humo kisha wanasingizia maafisa wa polisi kwamba ndio wanawahangaisha.

Kupitia ujumbe wa twitter, Rais huyo anayetetea kiti chake kwa muhula wa sita aliwaonya viongozi wa upinzani kuwa watakabiliwa vikali kwa kusababisha ghasia nchini humo kwa kuwashambulia “wafuasi wa National Resistance Movement (NRM).

“Uganda iko imara na serikali ya NRM haitawaruhusu wanaojaribu kuvuruga uthabiti kuepuka adhabu. Aidha, ningependa kuwaambia wale wanaowashambulia wafuasi wa NRM kwamba mtapoteza hiyo hamu. Mnafuata mkondo ambao tunaufahamu fika; vita,” akaonya Rais Museveni.

Bw Kyagulanyi aliachiliwa mnamo Ijumaa jioni baada ya kufikishwa kortini ambapo alikana mashtaka ya kuchochea fujo. Aliiambia korti kwamba, haoni sababu ya kufikishwa kortini kwa sababu hakuwa amefanya kosa lolote.

“Kwa maoni yangu, kesi hii haipasi kuwa kati ya Uganda na Kyagulanyi. Kwa hakika kesi inapasa kuwa ya Uganda dhidi ya Museveni. Museveni ndiye anapaswa kuwa kizimbani hapa kwa kuua raia wasio na hatia na kutenda uhalifu dhidi ya binadamu. Mheshimiwa nimefikishwa hapa sio kwa sababu nimetenda kosa lolote; niko hapa kwa sababu nimejitolea kukomesha udikteta wa miaka 35 nchini Uganda,” akasema Bw Kyagulanyi.

Jumamosi, jeshi lilitoa taarifa likisema litaendesha operesheni ya kupambana na waandamanaji na watu ambao wataamua kusababisha fujo nchini Uganda.