Kimataifa

Idadi ya waliouawa kwenye shambulizi la Boko Haram mazishini yaongezeka

July 30th, 2019 2 min read

Na AFP na MARY WANGARI

WATU 65 waliokuwa wakihudhuria mazishi walifariki mnamo Jumamosi, 27, kufuatia shambulizi la kigaidi lililotekelezwa na Boko Haram mjini Borno eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, idadi ya vifo ikiwa mara tatu ya idadi ya awali, ripoti zimesema.

Miili zaidi ya mamia ya watu ilipatikana mnamo Jumapili kufuatia shambulizi hilo lililotekelezwa siku iliyotangulia katika kijiji kimoja kilicho karibu na jiji kuu, Maiduguri.

“Ni watu 65 waliofariki na 10 wakajeruhiwa,” alisema Muhammed Bulama, mwenyekiti wa serikali eneo hilo.

Bulama alisema kwamba watu zaidi ya 20 walikuwa wamefariki katika shambulizi la awali katika mkutano wa mazishi.

Mamia waliuawa walipokuwa wakiwakimbiza washambulizi hao.

Kiongozi wa kundi kutoka eneo hilo linalopinga kundi la wapiganaji wa Boko Haram alithibitisha idadi ya waliofariki huku akitoa ripoti tofauti kiasi kuhusu shambulizi hilo.

“Watu 23 waliuawa walipokuwa wakirejea kutoka kwenye mazishi na wengine 42 waliosalia wakauawa walipokuwa wakiwafuata magaidi hao,” Bunu Bukar Mustapha alieleza AFP.

Bulama alisema alifikiri shambulizi hilo jipya lilikuwa juhudi za kulipiza kisasi dhidi ya mauaji ya wapiganaji 11 wa Boko Haram wiki mbili zilizopita yaliyotekelezwa na wakazi wakati wapiganaji hao walipovamia kijiji chao ambapo wakazi walinasa bunduki 10.

Buhari achemka

Mnamo Jumapili, Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alikosoa vikali tukio hilo na kuamrisha kikosi cha jeshi la anga pamoja na jeshi la nchi kavu kuwasaka washambulizi hao kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa afisi ya Rais.

Kundi la Boko Haram limekuwa likishambulia wilaya ya Nganzau mara kwa mara.

Kundi hilo la kigaidi limehangaisha eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria kupitia mashambulizi yaliyodumu kwa mwongo mmoja ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 27 000 huku watu zaidi ya milioni mbili wakifurushwa makwao.

Kundi hilo limegawanyika baina ya kundi la Boko haramu linaloegemea kiongozi wa jadi Abubakar Shekau na kundi la Iraq la Islamic State pamoja na kundi la Levant (ISIL ama ISIS).

Kundi la Shekau hulenga wahasiriwa wasio na uwezo wa kivita kama vile raia huku kundi la Islamic State West Africa Province (ISWAP) likivamia vikali vikosi vya kijeshi tangu mwaka 2018.