Habari Mseto

Idadi ya wanaokopesha pesa serikali yaongezeka

April 29th, 2024 1 min read

NA SIAGO CECE

IDADI ya Wakenya wanaokopesha serikali pesa imeongezeka licha ya hali ngumu ya kiuchumi. Wengi wanatumia njia hiyo kama mbinu za kupata riba ya juu katika uwekezaji wao.

Kulingana na wataalamu wa uwekezaji, ujuzi ulioenea wa masuala ya fedha, teknolojia na muda mfupi wa kurudisha pesa baada ya kuwekeza umesababisha idadi ya Wakenya wanaoikopesha serikali kuongezeka.

Mojawapo ya njia ambapo raia wanaweza kukopesha serikali pesa ni kupitia kwa ununuzi wa Treasury Bonds au Treasury Bills.

Katika mpango huu, serikali kupitia Benki Kuu ya Kenya inatoa mgao kama ‘hisa’ hivi na kualika wawekezaji wanunue kwa ajili ya kupata faida pamoja na mtaji baada ya kipindi fulani, chini zaidi kikiwa miezi mitatu. Kwa maana hii, mwekezaji anaipatia Serikali pesa kwa ajili ya kuvuna faida baada ya kipindi husika.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya GenAfrica, Patrick Kariuki, alisema Wakenya wengi wameongeza ujuzi wa kuwekeza pesa.

Wakati wa mahojiano, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Bungeni Ndindi Nyoro alisema ongezeko la uwekezaji wa mfumo huo lilitokana na kuimarika kwa uchumi wa Kenya.