Kimataifa

Idadi ya watoto walioathirika kutokana na mzozo wa kisiasa Venezuela yaongezeka

April 6th, 2019 1 min read

UMOJA WA MATAIFA

IDADI ya watoto ambao wameathirika kutokana na mzozo wa kisiasa nchini Venezuela ambao wanahitaji misaada ya kibinadamu mwaka 2019 inatarajiwa kuongezeka maradufu hadi kufikia watoto milioni 1.1 kutoka takriban watoto 500,000 Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) limesema.

Idadi hiyo inajumuisha watoto ambao waondolewa kutoka Venezuela, waliorejea na wengine walipata hifadhi miongoni mwa jamii mbalimbali katika maeneo ya Latin America na Caribbean, shirika hilo lilisema kwenye taarifa.

Takwimu hizo zinathibitisha matarajio miongoni mwa mashirika ya kutoa misaada kwamba mzozo wa kisiasa utaendelea kuwa mbaya zaidi katika miezi ijayo na hivyo yatahitaji kuimarisha usambazaji wa misaada kwa watoto na familia zitakazoathirika.

UNICEF ilitoa wito kwa serikali za mataifa ya eneo hilo kudumisha hali za watoto na kuhakikisha kuwa wanapata mahitaji ya kimsingi.

Ripoti moja iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na kufikiwa na wanahabari wa AFP ilisema kuwa watu milioni saba, sawa na asilimia 24 ya jumla ya idadi ya watu nchini Venezuela wanahitaji misaada ya kibinadamu kwani wanakosa chakula na huduma za kiafya.

Vikwazo

Rais Nicolas Maduro amesema changamoto za kiuchumi zinazoikabili Venezuela zinatokana na vikwazo vya kiuchumi iliyowekewa na Amerika.

Lakini kiongozi wa upinzani Juan Guaido, ambaye amejitangaza kuwa Rais, anasema matatizo hayo yanachangiwa na ufisadi serikalini na usimamizi mbaya wa rasilimali za umma. Kando na Amerika, mataifa mengine 50 yanaunga mkono Bw Guaido.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) linatarajiwa kufanya kikao wiki ujao, kufuatia ombi la Amerika, kujadili mzozo wa kibinadamu nchini Venezuela.