Idadi ya watu waliouawa na kimbunga Freddy, Malawi imefika 326

Idadi ya watu waliouawa na kimbunga Freddy, Malawi imefika 326

NA AFP

BLANTYRE, Malawi

IDADI ya watu waliokufa kutokana na kimbunga Freddy nchini Malawi imeongezeka hadi 326, Rais wa nchi hiyo Lazarus Chakwera amesema.

Idadi hiyo inafikisha idadi ya waathiriwa wa janga hilo nchini Malawi tangu Februari kuwa zaidi ya 400.

Kufiakia Alhamisi jioni waokoaji walikuwa wakiendelea kufukia miili huku uwezekano wa kupata manusura ukiwa finyu baada ya kimbunga hicho kurejea kupiga maeneo ya nchi kavu nchini humo kwa mara ya pili.

“Kufikia Alhamisi, idadi ya waliokufa kutokana na janga hilo ilipanda kutoka 225 hadi 326,” akasema Rais Chakwera alipozuru eneo la kusini mwa Malawi karibu na jiji la kibiashara, Blantyre mnamo Ijumaa.

“Idadi ya watu waliopoteza makazi imeongezeka zaidi ya maradufu hadi 183, 158 huku idadi ya familia zilizohama makwao ikitimu 40,702,” akaongeza.

Kwa mara nyingine Rais Chakwera alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuisaidia Malawi kutokana na madhara ya kimbunga hicho ambacho pia kilisababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Zaidi ya vibanda 300 vya muda vimejengewa manusura, huku wanajeshi na polisi wakitumika kusaidia katika shughuli za uokoaji na kuwasaidia manusura.

Rais Chakwera ametangaza wiki mbili za maombolezo na hali ya hatari nchini humo.

“Kimbunga hicho kimeharibu mali, makazi, mimea mashambani na miundomsingi yakiwemo madaraja. Kutokana na uharibifu huo, imekuwa vigumu kwa watoaji misaada kufikia jamii nyingi zilizoathirika,” Rais Chakwera akasema.

Kimbunga Freddy kwa mara ya kwanza kilishuhudiwa kusini mwa Afrika mwishoni mwa Februari, kikisababisha uharibifu Madagascar na Msumbiji kabla ya kuenea hadi nchi ya Malawi isiyopakana na bahari.

Baadaye, upepo huo ulivuma juu ya Bahari Hindi ambapo ulipata nguvu kabla ya kubadili mkondo na kugonga nchi kavu kwa mara ya pili.

Mvua imepungua tangu Jumatano lakini kimbunga Freddy bado kinavuma na kuelekea kushikilia rekodi ya kudumu kwa muda mrefu.

Nchini Msumbiji kimbunga hicho kilisababisha angalau vifo vya watu 73 huku makumi ya maelfu yaw engine wakipoteza makazi katika muda wa wiki kadha zilizopita.

Aidha, kilisababisha vifo vya watu wengine 17 katika kisiwa cha Madagascar.

Rais wa Musumbiji Filipe Nyusi pia ameomba msaada wa dharura kutoka jamii ya kimataifa ili taifa hilo liweze kujenga upya miundo msingi iliyoharibiwa na janga hilo katika mkoa wa Zambezia, unaopakana na Malawi.

Waokoaji nchini Malawi walikuwa na wakati mgumu kufukua miili iliyozikwa kwenye vifusi vya nyumba kwa kukosa mbwa wa kunusa na vifaa vya kisasa,isipokuwa sepetu.

Katika mji wa Manje, ulioko umbali wa kilomita 15 kusini mwa Blantyre, miili mitano ilipatikana na wakazi kwenye vifusi vilivyochanganyana na matope.

“Harufu kali katika eneo hili ni ishara tosha kwa maiti zimeona chini ya vifusi hivi,” akasema Rose Phiri, mkazi wa eneo hilo akitizama mashine ikichakura vifusi hivyo.

Watabiri wa hali ya anga wanasema kimbunga Freddy  kimedumu kwa muda mrefu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Wandayi awaomba waajiri kuwapa wafanyakazi ruhusa ya...

Jopo la IEBC latoa hakikisho la kuteua mwenyekiti kwa njia...

T L