Habari Mseto

Idara lawamani baada ya mbegu kukosa kuota

April 15th, 2019 1 min read

NA RICHARD MAOSI

WAKULIMA kutoka Bonde la Ufa wanalaumu Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa kwa kuwapotosha, ilipotangaza kuwa mvua kubwa ingenyesha wiki ya kwanza ya Aprili.

Kaunti zilizopata pigo ni Kericho, Uasin Gishu, Nakuru , Nyandarua na Kitale ambazo huchangia asilimia kubwa ya mazao kila mwaka humu nchini.

Mapema mwezi huu maeneo kadhaa yalishuhudia manyunyu ya mvua yaliyochochea wakulima kuandaa mashamba yao kwa msimu wa upanzi.

Lakini wiki chache baadaye hali ya kiangazi imerejea na kuzima matumaini ya wakulima kujaza maghala yao msimu huu.

Mbegu zilikosa kuchipuka na zile zilizoota zilinyauka mara tu unyevu ulipokosekana kwenye ardhi.

Aidha kiangazi kimechochea mito kukauka, na kuwaadhiri wakulima wanaoendesha ukulima kandokando ya chemchemi na vyanzo vya maji.

Kulingana taasisi ya utabiri wa hali ya anga duniani Goddad Institute for Space Studies (GISS), kiwango cha joto ulimwenguni kimeongezeka kwa nyuzijoto 0.8.

Hali hii inaendelea kuwa mbaya huku mabara yakiendelea kugeuka na kuwa majangwa hasa maeneo ya Afrika Magharibi na Kaskazini.

 

Hatua hii imewafanya baadhi ya wakulima kukisia huenda mwaka huu wasipate mazao ya kutosha kwa sababu ya ukosefu wa mvua.

Baadhi ya mashamba tuliyozuru, wakulima hawakuficha hofu yao waliposema kuwa taifa hili linaweza kukumbwa na baa la njaa la aina yake ifikapo 2020.

Naftali Mugo, mkulima wa mahindi na maharagwe kutoka eneo la Lanet, Kaunti ya Nakuru anasema aliamua kurudia ufugaji wa kuku bei ya mahindi ilipoanza kuteremka.

Alieleza haoni faida ya kupanda mahindi, ingawa sima ni lishe inayopendwa na asilimia kubwa ya watu humu nchini. Anasema ameweka akiba baadhi ya mahindi aliyovuna mwaka uliopita 2018 akisubiri yaishe.