Habari Mseto

Idara maalumu yaundwa kukabiliana na changamoto za ukame mbugani

July 26th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

KENYA inaendelea kupoteza ndovu wengi kutokana na ukame katika baadhi ya mbuga za wanyama.

Kulingana na Waziri wa Utalii na Wanyamapori, idadi ya wanyama wanaouawa na wawindaji haramu imepungua kwa iwango kikubwa.

Waziri Balala alisema Jumatano kuwa zaidi ya ndovu 440 walikufa mwaka 2017 kutokana na ukame na serikali imeweka juhudi za kuwaokoa wanyama hao.

“Ni kwa sababu hii serikali imeanzisha kitengo kipya cha Wildlife State Department ili kukabiliana na changamoto za ukame,” alisema waziri Balala.

Alizungumza alipomkabidhi Bw Patrick Kilonzo tuzo ya Head of State Commendation (HSC) aliyopewa na Rais Uhuru Kenyatta kwa juhudi zake za kuwa wa msaada mkubwa kwa wanyamapori.

 

Bw Patrick Kilonzo alipomtembelea Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Najib Balala katika afisi yake Julai 24, 2019. Picha/ Magdalene Wanja

Mwaka 2017 Bw Kilonzo aliibua hisia kwenye mitandao nchini na nchi zingine kwa juhudi zake za kuwapa wanyamapori maji wakati wa ukame licha ya hatari zilizopo mbugani.

Jambo ambalo Wakenya wengi hawakufahamu ni kwamba, Bw Kilonzo alikuwa anasumbuliwa na figo.

Kutokana na matendo yake, kampuni inayohusika na maji kutoka nchi ya India imejitolea kumlipia pesa zinazohitajika kwa matibabu yake nchini India.

Kampuni hiyo kwa jina Maithri Aquatech Private Limited pia imemzawadi Bw Kilonzo na mashine ya kuvuta maji kutoka hewani kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Bw Kilonzo anatarajiwa kwenda nchini India kupokea matibabu Agosti 2019.