Habari Mseto

Idara ya magereza yaagizwa imtengee nafasi mshukiwa mwenye kilo 150

May 16th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

IDARA ya Magereza ilitakiwa Jumanne iweke mipango ya malazi kwa mshukiwa mmoja wa ufisadi kutokana na uzani wake mkubwa wa kilo zaidi ya 150.

“Natahadharisha idara ya magereza ihakikishe kuwa James Mutua Nzuni amepewa makao mema kutokana na uzani wake,” hakimu mkuu Francis Andayi alisema Jumanne.

Bw Nzuni (pichani) alisindikizwa hadi mahakamani kwa mwendo wa kinyonga na afisa wa polisi .

“Hebu keti hapa,” Bw Nzuni alionyeshwa kiti na afisa wa polisi.

“Asante,” alisema huku akichukua muda mrefu kufikia kiti na kuketi.

Bw Nzuni mmwenye umri wa miaka 53 alikabiliwa na shtaka kupokea pesa Sh945,000  kwa njia ya udanganyifu akidai ataangalia kesi zilizokuwa zimekwama katika mahakama kuu,.

Mshtakiwa alikanusha mashtaka kisha akaomba aachiliwe kwa dhamana. Upande wa mashtaka haukupinga.

Alikana alipokea pesa hizo akijifanya angelichunguzia kampuni ya Ashut Engineering kesi zake katika mahakama kuu.

Alichiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh300,000 hadi Mei 23 kesi itakapotajwa.