Habari

Idara ya Uhamiaji yasitisha shughuli za kawaida za utoaji paspoti

November 7th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

IDARA ya Uhamiaji imesitisha, kwa muda, shughuli za utoaji paspoti mpya katika vituo vyake vyote nchini kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19.

Ni maombi ya dharura pekee yatashughulikiwa.

Vile vile, idara hiyo imesema kuwa imefutilia mbali miadi iliyowapa watu mbalimbali kuwasilisha fomu za maombi ya paspoti na usajili wa kielektroniki.

Wawasilishaji maombi ya kutaka paspoti kwa ajili ya kusafiri kwa shughuli za kimatibabu, masomo na kazi za serikali waliagizwa kuwasiliana na idara hiyo kupitia nambari ya dharura ya 0110 922 065 nyakati za kazi.

“Hii ni kulingana na agizo la serikali kuu kwamba shughuli zipunguzwe katika afisi za serikali kuzuia kuenea kwa Covid-19,” idara hiyo ikasema Ijumaa kwenye taarifa.

Watu wenye hitaji la dharura la kusafiri watahitajika kutoa stakabadhi ili waweze kuhudumiwa.

Mnamo Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta aliamuru kwamba afisi zote za serikali kuu zipunguze shughuli zinazohitaji wafanyakazi kufikia afisini, ili kuzuia misongamano.

Aliagiza idara zote za serikali kuu na zile za kaunti kuhakikisha kuwa ni wafanyakazi wanaotekeleza majukumu muhimu zaidi pekee ndio wanaruhusiwa kufika katika afisi huku wengine wakifanya kazi wakiwa nyumbani.

“Wafanyakazi wenye umri wa miaka 58 kwenda juu na wale wenye matatizo ya kiafya pia wanafaa kufanya kazi wakiwa nyumbani. Masharti kama haya yanalenga kuzuia kuenea kwa virusi vya corona hali ambayo imeongezeka zaidi katika mwezi wa Oktoba,” akasema Rais Kenyatta kwenye hotuba kwa taifa.