Habari Mseto

Idara yatabiri kutakuwa na mvua kubwa Pwani hadi Ijumaa

September 26th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

MVUA kubwa imetabiriwa kunyesha kuanzia Jumatano hadi Ijumaa katika maeneo ya Pwani.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Jumanne ilitoa ilani kwamba mvua hiyo itaandamana na upepo mkali na mawimbi makubwa baharini na ikashauri wakazi na wavuvi kuwa waangalifu.

Kaunti ambazo zitaathirika na hali hii ya hewa ni Kwale, Mombasa, Kilifi, Taita Taveta, Lamu na Tana River.

“Wakazi katika maeneo hayo wanashauriwa kujihadhari na mafuriko ya ghafla,” ikasema ilani hiyo, ambayo iliongeza kuwa mvua hiyo itapungua Ijumaa.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini, Bi Stella Aura, alisema maeneo mengine ya nchi pia yanatarajiwa kushuhudia mvua katika kipindi cha siku saba kuanzia leo japo si kwa kiasi kikubwa kama Pwani.

“Ukanda wa Pwani unatarajiwa kushuhudia mvua katika maeneo kadhaa katika kipindi chote cha utabiri huu. Mvua kubwa inatarajiwa kuanzia Jumatano hadi Ijumaa,” akasema Bi Aura.

Alieleza kuwa mbali na Pwani, imetabiriwa mvua itakuwa ikinyesha masaa ya mchana pekee katika maeneo kadhaa yanayopakana na Ziwa Victoria, nyanda za juu za Rift Valley ya Kati, Magharibi na Kusini, eneo la Kati na Kaskazini Mashariki.

Mvua za vuli zinatarajiwa kuanzia mwezi Oktoba.