Habari

Idara yatahadharisha mvua kubwa kunyesha mwezi huu

March 2nd, 2020 2 min read

Na COLLINS OMULO

WAKENYA wametakiwa kujiandaa kwa ajili ya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia mwezi huu wa Machi.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ilisema kuwa kiwango cha mvua kitakuwa kubwa zaidi Aprili katika maeneo yote ya nchi isipokuwa Pwani ambapo kiwango kitakuwa cha juu zaidi Mei.

Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, Bi Stella Aura alisema kuwa mvua kubwa inatarajiwa katika maeneo ya Magharibi, Pwani, Kaskazini Mashariki, Kati na upande wa Mashariki.

Hata hivyo, maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Kenya, kama vile Turkana, yatakuwa na kiwango cha kawaida cha mvua.

Kulingana na Bi Aura, mvua kubwa inatarajiwa kuanzia wiki hii katika maeneo ya Pwani, Magharibi, nyanda za Kati na Bonde la Ufa. Maeneo mengine ya nchi yataanza kupokea mvua wiki ya tatu na nne ya mwezi huu.

Alisema kuwa maeneo ya Kati na magharibi mwa Kenya yalipokea kiasi kikubwa cha mvua Februari.

Mvua iliyonyesha katika maeneo ya kusini mwa Bonde la Ufa, yakiwemo maeneo ya Narok na Kajiado mwezi uliopita, itaendelea mwezi huu alieleza

Mvua hiyo alisema Bi Aura itaendelea kunyesha katika kaunti za Ukanda wa Ziwa kama vile Homa Bay, Siaya, Kisumu, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma na Busia.

Hali sawa na hiyo itashuhudiwa katika Kaunti ya Nakuru, Laikipia na Baringo japo wiki ijayo kutakuwa na vipindi vya jua.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa katika maeneo ya Nairobi, Nyandarua Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka Nithi; mvua itaanza kunyesha wiki hii. Kutakuwa na vipindi vya jua wiki ijayo na mvua itaanza kunyesha tena wiki ya tatu na nne ya mwezi huu.

Vilevile, alisema Kaunti za Kusini Mashariki mwa nchi kama vile Machakos, Makueni, Kitui, Taita Taveta na baadhi ya sehemu za Tana River zitapokea mvua wiki hii.

“Mvua itakatika wiki ijayo kabla ya kuanza tena wiki ya tatu na nne ya mwezi huu. Hali sawa na hiyo itashuhudiwa katika maeneo ya Mombasa, Kwale na Kilifi,” alisema.

Aliongeza, “Maeneo ya Lamu, sehemu za kaskazini mwa Kilifi na baadhi ya sehemu za Tana River, zitaanza kupokea mvua kubwa wiki ya tatu na nne ya mwezi huu.”

Kadhalika, Bi Aura alisema kuwa maeneo ya Turkana, Pokot Magharibi na Samburu yataanza kupokea mvua kubwa wiki ya nne ya mwezi huu na mwanzoni mwa Aprili.

Maeneo ya Wajir, Isiolo, Garissa, Mandera na Marsabit yatapokea mvua wiki ya tatu na nne ya mwezi huu.