Habari

Idd bila swala misikitini wala shamrashamra yakosa ladha

May 25th, 2020 2 min read

KALUME KAZUNGU na SHABAN MAKOKHA

WAISLAMU nchini Jumapili waliadhimisha Sikukuu ya Idd bila shamrashamra nyingi kufuatia kanuni zilizowekwa ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa kawaida wakati wa sherehe hii inayoadhimishwa baada ya kumaliza mwezi wa Ramadhan, Waislamu hufika kuswali kwa pamoja, kujumuika na jamaa na marafiki na kutakiana heri njema.

Katika Kaunti ya Lamu, misikiti yote ilisalia kufungwa huku maeneo ya ufuo wa Bahari Hindi eneo la Lamu ambayo mara nyingi hufurika Waislamu wakiadhimisha Idd, mwaka huu walibakia katika nyumba zao kusherehekea Idd na kutii sheria za Covid-19, ikiwemo kujiepusha na mikutano na kutembea kwa makundi.

Akitangaza Jumamosi jioni kuwa Idd itasherehekewa jana, Kadhi Mkuu Ahmed Muhdhar alihimiza Waislamu kuzingatia masharti yaliyowekwa na serikali ili kudhibiti maambukizi.

Baadhi ya viongozi wa dini na wakazi waliozungumza na wanahabari walieleza masikitiko yao kuhusiana na jinsi virusi vilivyobadilisha mambo.

Ustadh Mohamed Abdulkadir alimuomba Rais Uhuru Kenyatta kuandaa kikao na viongozi wa dini kote nchini ili kujadili jinsi misikiti na makanisa yanavyoweza kufunguliwa hivi karibuni ili waumini waendeleze ibada zao.

Ustadh Abdulkadir alisema wako tayari kutii sheria zote zinazotolewa na wizara ya Afya ili kuzuia maambukizi au kuenea kwa Covid-19 ilmradi misikiti na makanisa yafunguliwe.

“Tunasherehekea Idd-Ul-Fitr leo kwa upweke mkubwa. Misikitini hakuendeki, matembezi au mikutano ya aina yoyote pia haifanyiki. Huu ni wakati ambapo waumini na familia hutembeleana. Idd-Ul-Fitr pia hutumika sana kuwatembelea wasiojiweza na kuwasaidia,” alisema.

“Kwa sasa hayo yote hayafanyiki. Ninamsihi Rais Kenyatta kuandaa kikao na viongozi wa madhehebu yote nchini ili tujadiliane na maeneo ya kuabudia yafunguliwe. Kukatazwa kuomba misikitini au makanisani si jambo la busara kamwe,” akasema Bw Abdulkadir.

Waislamu wasiojiweza mjini humo pia walitunukiwa nguo na wauzaji mitumba. Taifa Leo ilishuhudia wateja wakimiminika kwa wingi kwenye soko la Uwanja wa Kibaki mjini Lamu ili kujichukulia msaada huo wa nguo.

Msemaji wa wafanyabiashara hao, Bw James Babzii, alisema si mara ya kwanza kwao kuwatunuku wateja wao mitumba ya bure ili kuwasaidia wakati huu wa sherehe za Idd.

Mjini Mumias katika Kaunti ya Kakamega, Sheikh Omar Athman wa msikiti wa Sheikh Khalifa, alihimiza waumini kuangalia njia mbadala za kusherehekea sikukuu hiyo.

“Tunaposherehekea Idd, tufikirie kuhusu njia tofauti za kusherehekea, kwa mfano kupiga simu kwa njia ya video kuwasiliana na jamaa na marafiki. Ni muhimu kuwa salama na kuwalinda wengine tunaposherehekea siku hii,” alisema.

Alieleza kuwa janga lililopo, linahitaji kila mmoja kujitolea na kuhimiza Waislamu kukumbatia mbinu zilizowekwa za kukabili maambukizi ya virusi.