Habari Mseto

Idd-ul-Adha: Usalama waimarishwa Lamu

August 21st, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

USALAMA umeimarishwa katika kisiwa cha Lamu na maeneo yote ya mpakani mwa Lamu na Somalia wakati huu ambapo waumini wa dini ya kiisalmu wanaadhimisha sherehe ya IddulAdha kote ulimwenguni.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono (pichani) anasema tayari wamesambaza maafisa wa kutosha wa usalama kila sehemu ambapo waumini wa dini ya kiisalmu wanakongamana kwa sherehe za IddulAdha.

Akizungumza  na Taifa Leo mjini Lamu Jumanne, Bw Rono alisema pia wamehakikisha kila  maeneo ambayo  yamekuwa yakilengwa na magaidi wa Al-Shabaab, hasa Basuba, Milimani, Mangai, Mararani  na hata sehemu za  mpakani, ikiwemo Kiunga na na Ishakani zinalindwa ipasavyo.

Aidha aliwashauri wakazi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha usalama kwenye maeneo yao  unadhibitiwa.

“Tayari tumeweka  usalama wa kutosha hasa kisiwani Lamu ambapo waumini wa dini ya kiislamu  ni wengi. Tutahakikisha doria zinafanywa misikitini, mahotelini,  barabarani, baharini na hata angani. Ninawashauri wakazi kupiga ripoti kwa polisi iwapo watashuhudia tukio au mtu yeyote wanayemshuku kuwa  kero kwa  usalama,” akasema Bw Rono.

Aliwashauri wakazi kuukumbatia mfumo wa Nyumba Kumi katika kukabiliana na wahalifu hasa  msimu huu wa IddulAdha, ambapo k wageni wengi wanatarajiwa kuwasili Lamu kuadhimisha hafla hiyo.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo kisiwani Lamu aidha walisema wamefurahia jinsi usalama ulivyodhibitiwa kote Lamu.

IddulAdha ni hafla muhimu kwetu sisi waislamu. Tunawakumbuka wenzetu walioenda kuhiji. Hii ni nguzo muhimu ya imani kwetu waislamu. Pia tunashukuru serikali kwa kudhibiti usalama eneo hili,” akasema Bw Mohamed Bashauf.