IEBC huru kuandaa uchaguzi- Korti

IEBC huru kuandaa uchaguzi- Korti

JOSEPH WANGUI na LEONARD ONYANGO

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), sasa iko huru kuendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, baada ya mahakama kuondoa vikwazo.

Mahakama Kuu imeruhusu IEBC kuendelea na mchakato wa kutoa kandarasi ya vifaa vya kielektroniki vya kutambua wapigakura na kupeperusha matokeo (Kiems).Jaji Jairus Ngaah alitupilia mbali uamuzi wa Bodi ya Usimamizi wa Kandarasi za Umma (PPARB), ambayo ilibatilisha kandarasi iliyotangazwa na IEBC mapema mwaka huu.

IEBC ilitangaza kandarasi ya Kiems mnamo Mei 14, na kampuni tano za kimataifa zilituma maombi.Lakini bodi ya PPARB inayoongozwa na Bi Faith Waigwa, iliharamisha tenda hiyo mnamo Septemba 1, 2021, huku ikisema kuwa kampuni za Kenya zilibaguliwa.Bodi hiyo iliagiza IEBC kutangaza upya kandarasi hiyo ndani ya siku 30.

Kampuni ya Risk Africa Innovates Limited, ndiyo iliwasilisha malalamishi kwa PPARB ikidai kubaguliwa.IEBC ilizingatia agizo hilo na kutangaza tena kandarasi hiyo mnamo Septemba 22, lakini ikasitisha tena mchakato huo Oktoba 8, baada ya kampuni ya Risk Africa Innovates Limited kwenda katika Mahakama Kuu.

Lakini Jaji Ngaah katika uamuzi wake alikosoa bodi kwa kufutilia mbali mchakato huo huku akisema kuwa kampuni ya Risk Africa Innovates Limited, haikuwa miongoni mwa kampuni zilizotuma maombi ya kutaka kupewa kandarasi hiyo.

Jaji Ngaah alisema kuwa kampuni hiyo haikufaa kupeleka malalamishi katika bodi kwani haikuwa imetuma maombi.“Kampuni hiyo ililenga kupotezea IEBC wakati kwani haikuwa na haki ya kupeleka malalamishi yake mbele ya bodi,” akasema Jaji Ngaah.

Hiyo inamaanisha kuwa IEBC itaendelea na mchakato wake wa kutoa kandarasi ya kununua vifaa vya kutambulisha wapigakura kielektroniki.Mahakama ilibaini kwamba kampuni ya Risk Africa Innovates Limited, ilijaribu kutuma maombi baada ya makataa yaliyowekwa na IEBC kukamilika.

Kampuni za kimataifa zilizotuma maombi ya kutaka kusambaza vifaa hivyo ni Indra Soluciones Tecnologias De La Informacion, Smartmatic International Holding B.V, Genkey Solutions BV, Laxton Group Limited na Africa Infrastructure Development.

“Mtu anayetuma maombi ya kandarasi baada ya makataa kukamilika hatambuliwi hivyo hawezi kupeleka malalamishi kwa bodi akidai kubaguliwa,” akasema Jaji Ngaah.Katika uchaguzi wa 2017, IEBC ilitumia vifaa hivyo vya kielektroniki vilivyonunuliwa na kampuni ya Idemia, ambayo awali ilijulikana kama OT-Morpho.

Baadhi ya vifaa vya Kiems vilivyotumika katika uchaguzi uliopita, vilifeli na kusababisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta kufutiliwa mbali na Mahakama ya Juu

You can share this post!

Matumaini Achani huenda akapeperusha UDA Kwale

Ufisadi, ulafi vinasababisha majumba kuporomoka

F M