Habari Mseto

IEBC ilipoteza Sh9.5b katika uchaguzi 2017 – Ripoti

October 11th, 2018 2 min read

Na SAMWEL OWINO

WAKENYA walipoteza Sh9.5 bilioni katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana kupitia kwa ununuzi wa bidhaa na uagizaji wa huduma.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa mchunguzi mkuu wa hesabu za serikali Bw Edward Ouko.

Kulingana naye, pesa hizo zilipotea wakati wa uchaguzi wa Agosti 8 na uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.

Ripoti hiyo ya mwaka wa kifedha wa 2017/2018 uliokamilika Juni na iliyowasilishwa Bungeni Jumanne jioni inaonyesha kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haiwezi kutoa hesabu ya ilivyotumia fedha hizo.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kulikuwa na uharibifu mkubwa wa pesa za umma kupitia kwa ununuzi wa vifaa vilivyonunuliwa na tume hiyo kwa mamilioni ya fedha ambavyo havikuwasilishwa licha ya kulipiwa, au viliwasilishwa lakini havikutumiwa.

Bw Ouko alisema licha ya Sh47 milioni kutumiwa kununua betri za mashine za kunakili data wakati wa uchaguzi (BVR) Januari 2017, betri hizo hazijawahi kutumiwa. Alisema hakuna sababu yoyote iliyotolewa kuhusiana na hatua hiyo.

Uchunguzi huo unaonyesha kuwa IEBC ilinunua kiasi kikubwa cha data wakati wa uchaguzi wa Agosti (149,640.5 GB) kwa Sh127, 625,926 milioni ingawa ni 605.3 GB iliyotumiwa.

Data hiyo ilinunuliwa kutoka Safaricom, Airtel na Telkom.

Tume hiyo wakati huo ilinunua kadi 515 za simu kwa uchaguzi wa marudio ambazo hazikuwasilishwa na kusababisha kupotea kwa Sh4.5 milioni.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa IEBC ilitumia vibaya vifaa 1,000 vya data na kadi za simu zilizokuwa na masalio ya data.

Vifaa vya kwanza 700 na 300 aina ya Thuraya na kadi za simu zilizokuwa na data vilitolewa na kusambazwa katika maeneobunge kabla ya uchaguzi huo mkuu.

Hata hivyo, ni vifaa (modem) 339 vilivyotumiwa na kadi zilizokuwa na masalio ya 4GB.

Kutokana na hayo, Sh119.7 milioni hazijulikani zilivyotumika kulingana na ripoti hiyo.

Kulingana na ripoti hiyo, IEBC ilinunua masanduku 42,927 zaidi ya kupigia kura kwa uchaguzi wa marudio kwa Sh2,500 badala ya Sh2,250 zilizopendekezwa na muuzaji, na kusababisha kupotea kwa Sh10 milioni.

Katika utoaji wa taa za gesi zilizotarajiwa kutumika wakati wa uchaguzi wa Agosti 2017, ripoti hiyo ilisema kandarasi ilitolewa kwa njia isiyofaa kwani mwanakandarasi aliyepewa kandarasi hiyo hakutoa sampuli kama ilivyotangazwa katika tenda.

“Rekodi zinaonyesha kuwa tume hiyo haikuondoa kampuni hiyo kutoka kwenye utaratibu lakini iliipa kandarasi nyingine ya kutoa taa hizo kwa Sh5.5 milioni kinyume cha sheria,” alisema Bw Ouko.

Pia ripoti hiyo inaonyesha kuwa kuna tofauti ya hesabu ya taa ambazo IEBC ilitoa kwa maeneobunge na zilizobakia kwa stoo zake.

Tume hiyo pia inashutumiwa kuhusu kutoa malipo zaidi ya ilivyofaa katika kandarasi ya ununuzi na uwasilishaji wa beji.