Habari Mseto

IEBC ilivunja sheria kuhusu ununuzi – Bunge

October 31st, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumanne waliisuta Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kupeana zabuni ya ununuzi wa mitambo 45,000 ya kieletroniki ya thamani ya Sh6.4 bilioni iliyotumika kwa uchaguzi wa mwaka 2017 bila kufuata sheria.

Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) ilisema hatua ya tume hiyo kutoa zabuni ya moja kwa moja kwa kampuni ya Saphran Morpho, kutoka Ufaransa, ilikiuka sheria kuhusu usimamizi wa fedha za umma 2012 na ile ya ununuzi wa bidhaa za umma ya 2015.

“Inasikitisha kuwa hivi ndivyo maafisa wakuu katika IEBC waliiba pesa za umma kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali zilizowasilisha bidhaa na huduma zilizotumika katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8 na marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 29 mwaka jana. Sharti wawajibikie kosa hili,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Opiyo Wandayi.

Juhudi za Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Marja Hussein Marjan kujaribu kuwashawishi wabunge hao kwamba tume hiyo ilichukua hatua hiyo ili kutimiza makataa ya maandalizi ya uchaguzi hazikufaulu.

“Mbona zabuni ya thamani kubwa kiasi hiki ilipewa kampuni ya Saphran Morpho bila kushindaniwa ilhali kulikuwa na kampuni zingine nyingi ambazo zilihitimu kwa kazi hiyo? Sababu kwamba hakukuwa na muda wa kutosha kufuata taratibu zote za kutangaza na kupeana zabuni haina mashiko kwa sababu ni wazi kuwa IEBC ilikiuka sheria,” akasema Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Kulingana na Bw Nyoro, utoaji wa zabuni kwa njia ya moja kwa moja unaweza tu kufanywa ikiwa hakuna kampuni nyingine inayoweza kutoa bidhaa au huduma zinazohitajika.

Bw Marjan alisema uamuzi huo wa kupeana zabuni hiyo moja kwa moja kwa Saphran Morpho ulifanywa na aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wakati huo, Bw Ezra Chiloba, akifafanua makamishna hawakuhusika katika zoezi hilo.

“Uamuzi huo ulifanywa na Bw Chiloba na kazi ya makamishna wa tume ilikuwa ni kuhakikisha vifaa vilivyohitajika vimenunuliwa kwa wakati uliowekwa kulingana na mwongozo wa ununuzi,” akasema.

Bw Marjan, ambaye alikuwa ameandamana na kamishna Boya Molu pamoja na maafisa wengine wa IEBC, alikuwa akijibu maswali kutoka kwa wanachama wa PAC kuhusu hitilafu za matumizi ya fedha katika tume hiyo katika mwaka wa kifedha kufikia Juni 30, 2017.

Hitilafu hizo zimeorodheshwa katika ripoti ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Edward Ouko ya mwaka kifedha za 2016/2017.

Wabunge pia walilalamikia hatua ya IEBC kulipa madeni ya kima cha Sh2.4 bilioni bila kuwasilisha vocha za malipo inavyohitajika kisheria.

Katika malipo hayo, ilibainika kuwa mawakili waliokodiwa kwa huduma mbali za kisheria walilipwa jumla ya Sh450 milioni kabla ya uchaguzi mkuu Agosti 8.