Habari Mseto

IEBC isalie na makamishna saba, KNHRC yapendekeza

June 18th, 2019 2 min read

 Na CHARLES WASONGA

TUME ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR) imepinga pendekezo la kupunguzwa kwa idadi ya makamishna wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutoka saba hadi watano, ikisema hatua hiyo itaaathiri utendakazi wa tume hiyo.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bi Kagwiria Mbogori, jana aliwaambia wabunge wanachama wa Kamati inayosimamia utekelezaji wa Katiba (CIOC) kwamba idadi ya makamishna hao inapasa kusalia saba kama ilivyo chini ya sheria ya sasa.

“Kutokana na majukumu makubwa ya IEBC kama vile uendeshaji na usimamizi wa chaguzi, uainishaji upya wa mipaka pamoja na wajibu wa kutoa ushauri kuhusu sera kuhusu aina mbalimbali za chaguzi, tume hii haipasi kuwa na makamishna wanaopungua saba,” akasema Bi Mbogori kwenye wasilisho lililosomwa kwa niaba yake na mkurugenzi wa utafiti katika tume hiyo, Bi Anne Okutoyi.

KNCHR ilitoa mifano ya mataifa jirani ya Afrika kama vile Afrika Kusini, Malawi, Ghana, Uganda na Tanzania ambayo tume zao cha uchaguzi zina angalau makamisha saba, idadi inayolingana na majukumu ya tume hizo.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Ndaragwa, Bw Jeremiah Kioni, ilikuwa ikipokea maoni na mapendekezo ya tume hiyo ya haki kuhusu mswada unaolenga kuifanyia mageuzi sheria ya IEBC kwa lengo la kupunguza idadi ya makamishna kutoka saba hadi watano.

Mswada huo ambao uliwasilishwa bungeni mnamo Mei 5, 2019, pia unapendekeza kuundwa kwa jopo maalum, na la kudumu, la kuendesha shughuli ya uteuzi wa makamishna wa IEBC.

Jopo hilo pia litaendesha mchakato wa kujaza nafasi za makamishna ambao watajiuzulu kwa sababu mbalimbali kabla ya muda wao wa kuhudumu kukamilika.

Kuhusu kuundwa kwa jopo hilo tume ya KNCHR inapendekeza uwepo wa uwakilishi kutoka kwa walemavu, wanawake, vijana na watu kutoka jamii zilizotengwa kando na wawakilishi wa asasi zingine.

“Watu kama hawa watawakilisha sauti za idadi kubwa ya Wakenya ambao huwa hawapati nafasi katika asasi mbalimbali za umma. Hii ni muhimu kwa sababu IEBC ndio tume inayosimamia viongozi watakaounda sheria na sera za uongozi wa taifa hili,” akasema Bi Mbogori huku akiongeza kuwa jopo hilo lapaswa kuwa na wanachama 11.

Hata hivyo, Bw Kioni na wanachama wa kamati yake walitofautiana na pendekezo la KNCHR kuhusu idadi ya makamishna wakisema idadi iliyopendekezwa katika mswada huo ni bora.

“Endapo majukumu ya makamishna na afisi yatatenganishwa ipasavyo, bila shaka IEBC inapasa kuwa na makamishna wachache hata kuliko watano kama ilivyopendekezwa katika mswada huu. Isitoshe, wakati huu kuna makamishna watatu pekee na wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila shida,” akasema Bw Kioni.