IEBC kufanya usajili tena Januari 2022

IEBC kufanya usajili tena Januari 2022

Na WALTER MENYA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itaendesha awamu ya pili ya usajili wa wapigakura kwa wingi mnamo Januari 2022 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao.

Akiongea Ijumaa katika mkutano wa kila mwaka wa Chama cha Wahariri Nchini (Kenya Editors Guild), Naivasha, kaimu afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Hussein Marjan alifichua kuwa tume hiyo imepokea Sh8.7 bilioni kutoka kwa Hazina ya Kitaifa kufadhili shughuli hiyo.

“Pesa hizo zitagharimia awamu ya pili ya usajili wa wapigakura kwa wingi kuanzia Janauri. Pesa hizo ni sehemu ya bajeti ya Sh40.9 bilioni za kuendesha uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema.

Licha ya kuongezewa pesa zaidi, Bw Marjan hata hivyo alisema IEBC bado inakabiliwa na upungufu wa bajeti wa Sh5.1 bilioni.Katika awamu ya kwanza ya shughuli hiyo iliyoendeshwa kuanzia Oktoba 4 hadi Novemba 5, 2021, IEBC iliwasajili wapigakura 1.5 milioni pekee japo ililenga kuwasajili wapigakura wapya milioni sita.

Wapigakura hao 1.5 milioni walikuwa kando na wapigakura wapya 180,938 waliosajiliwa kati ya Oktoba 15, 2018 na Agosti 31, 2021, kupitia shughuli ya kawaida ya usajili wa wapiga.

Usajili huo huendeshwa katika afisi za IEBC katika ngazi ya maeneo bunge na kaunti.

Ukaguzi

“Tume inaendelea na mpango wa kukodi kampuni huru ambayo itakagua sajili ya wapiga kura. Wapigakura watakagua sajili hiyo ili kuthibitisha iwapo maelezo yao ni sahihi. Ukaguzi huo utafanya kwa muda wa siku 30, angalau siku 60 kabla ya tarehe ya uchaguzi,” akasema Bw Marjan.

Wakati huo huo, tume hiyo imetangaza kuwa inapanga kuendesha usajili wa wapiga kura wapya katika mataifa ya ng’ambo.

Mataifa yanayolengwa ni; Uingereza, Canada, Amerika, Sudan Kusini, Qatar, Milki ya Umoja wa Kiarabu (UAE) na Ujerumani.

Hii inaongeza idadi ya nchi za nje ambako Wakenya wataweza kupiga kura kufikia 11.

Katika uchaguzi mkuu wa 2017 ni Wakenya katika mataifa ya Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, na Afrika Kusini pekee walioshiriki katika uchaguzi wa urais pekee.

Jumla ya idadi ya wapigakura katika nchi hizo ilikuwa 4,393.

Uamuzi wa kuongeza nchi sita zaidi katika orodha ya nchi za kigeni ambako Wakenya watapiga kura huenda ikachangia wagombeaji urais kuweka mikakati ya kusaka kura katika nchi hizo.

Hii ni kwa sababu katika hali ambapo ushindani utakuwa mkali, kura hizo huenda zikaaamua mshindi katika kinyang’anyiro cha urais.

You can share this post!

Majukumu ya AG yagawiwe Waziri – Korti

Kingi afunguka roho kuhusu PAA, uhusiano wake na Raila

T L