Habari Mseto

IEBC kuhamisha makao yake mbali na jiji kuhudumu bila bughudha

May 31st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) inahamisha afisi zake kuu kutoka Jumba la Annniversary, Nairobi, na kuzipeleka mbali na katikati mwa jiji (CBD).

Kulingana na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, hatua hiyo inalenga kuliwezesha shirika hilo kutekeleza majukumu yake bila kutatizwa.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria jana, Bw Chebukati alisema tume hiyo inalenga kununua au kujenga jumba litakalokuwa afisi zake kuu nchini.

Alisema hatua hiyo itawezesha shirika hilo kukomboa fedha za wananchi ambazo hutumiwa kukodisha makao yake katikati mwa jiji. “Tume imo katika harakati za kuhamisha makao yake kutoka Jumba la Anniversary kuyapeleka mbali na katikati mwa jiji. Tunataka kumiliki jumba letu,” alisema.

Aliongeza kuwa hatua hiyo itahakikisha tume hiyo haitatazika au kuvuruga biashara za watu wengine, kama ambavyo umekuwa mtindo wakati wa maandamano.

“IEBC ni shirika huru ambalo lina majukumu mengi na wakati mwingi, watu ambao hawajaridhika hutaka kuandamana,” alisema.