IEBC: Mchakato wa kuteua makamishna 4 wapya kushika kasi wiki hii

IEBC: Mchakato wa kuteua makamishna 4 wapya kushika kasi wiki hii

Na CHARLES WASONGA

ASASI mbalimbali ambazo zinahitajika kuwasilisha majina kwa jopo la kuteua makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zinatarajiwa kuwasilisha wateule wao wa kufanya kazi hiyo kwa afisi ya Rais leo Jumatano, Aprili 21, 2021.

Hatua hii itatoa nafasi kwa mchakato wa kuwateua makamishna wanne wapya katika tume hiyo kuanza baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza rasmi nafasi hizo kuwa wazi.

Mnamo Aprili 14, 2021, Rais Kenyatta alitangaza nafasi za Paul Kurgat, Consolata Nkatha, Margaret Mwachanja na Dkt Roselyn Akombe kuwa wazi kupitia ilani kwenye gazeti rasmi la serikali.

Kulingana na Sheria ya IEBC iliyofanyiwa marekebisho, Tume ya Huduma za Bunge (PSC) inahitaji kuteua watu wanne katika jopo hilo la uteuzi; wanawake wawili na wanaume wawili.

Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) chapaswa kuteua mtu mmoja na Baraza la Madhehebu Mbalimbali Nchini (Inter Religious Council) likiteua wawakilishi wawili katika jopo hilo la watu saba.

Asasi hizo zinatarajiwa kuwasilisha majina ya wawakilishi wao kwa Rais Kenyatta ambaye atawateua rasmi kulingana na sheria hiyo ya IEBC iliyofanyiwa mabadiliko Oktoba 2020.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ambaye ni mwenyekiti wa JSC alisema tume hiyo itafanya kikao Alhamisi wiki hii kujadili jinsi itagawa nafasi hizo nne.

You can share this post!

Jubilee kuvunja uhusiano na PDR ambacho sasa ni UDA

Timbe kutafuta mwanzo mzuri nyumbani Vissel Kobe na...