IEBC na Kihara wakata rufaa kunusuru BBI

IEBC na Kihara wakata rufaa kunusuru BBI

Na WALTER MENYA

JUHUDI za kuokoa mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) zimefikishwa rasmi katika Mahakama ya Juu.

Hii ni baada ya Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwasilisha ilani tofauti za kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa wa kuzima mchakato huo.

Bw Kihara amebaini sababu nane ambazo anatarajiwa kutegemea kubatilisha uamuzi huo uliotolewa na jopo la majaji saba wa mahakama hiyo wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo Daniel Musinga.

Kwa upande wake tume ya IEBC itategemea sababu tatu kupinga kauli ya majaji hao kwamba haikuwa na idadi tosha wa makamishna iliposhughulikia mswada huo wa marekebisho ya Katiba.

Katika rufaa yake, Mwanasheria Mkuu anataka Mahakama Kuu kufafanua wazi kuhusu sera ya muundo wa asasi za kiutawala inayozuia marekebisho ya vipengele fulani vya katiba kupitia idhini ya umma.

Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa zilishikilia, katika maamuzi yao, sera hiyo haikuzingatiwa na kamati shikilizi iliyoendesha mchakato wa BBI.

Hata hivyo, Bw Kihara anapinga msimamo huu. “Uchanganuzi wetu unaonyesha kuwa kihistoria, sera hiyo imetumika tu wakati ambapo, na katika hali ambapo, raia hawahusishwi moja kwa moja kupitia kura ya maamuzi.

Pili, Katiba yetu tayari ina vipengele kadhaa vinavyolinda muundo wake wa kimsingi,” wakili mkuu wa serikali Kennedy Ogeto akasema.

Mbali na Jaji Musinga, majaji wengine waliotoa uamuzi huo ni Roselyn Nambuye, Patrick Kiage, Gatembu Kairu na Francis Tuiyott.

Hata hivyo, majaji Hannah Okwengu na Fatuma Sichale walitofautiana na wenzao watano kuhusiana na suala hilo.

Nafasi ya Rais katika marekebisho ya katiba ilikuwa suala jingine tata katika maamuzi ya Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu.

Kulingana na afisi ya Mwanasheria Mkuu, “Hakuna kipengele katika Katiba kinachomzuia Rais kuanzisha marekebisho kwenye Katiba kwa kusaka idhini ya umma.”

“Kwa mtazamo wetu, Rais kama raia yeyote ana haki za kiraia na kisiasa, ikiwemo haki ya kuanzisha marekebisho ya katiba kwa kupitia idhini ya umma,” Bw Ogeto.

Mwanasheria mkuu pia atataka majaji saba wa Mahakama ya Juu kuamua ikiwa pendekezo la BBI la kubuni maeneobunge 70 zaidi linatii katiba au la.

Kuhusu suala hilo, Mahakama ya Rufaa ilisema kuwa wajibu wa kubuni maeneobunge zaidi ni wa IEBC, inavyoelezwa katika kipengele cha 89 cha Katiba.

Kwa upande wake, IEBC ambayo sasa ina idadi tosha ya makamishna baada ya kuapishwa makamishna wapya saba, inasema kuwa katiba inairuhusu kuendesha shughuli zake ikiwa na makamishna watatu.

Lakini kulingana na maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, IEBC haikuwa na idadi hitajika ya makamishna ilipofanya maamuzi kuhusu mchakato wa marekebisho ya katika kupitia BBI.

Tangu Aprili 2018, tume hiyo imekuwa ikiendesha shughuli zake na makamishna watatu pekee; mwenyekiti Wafula Chebukati, Prof Abdi Guliye na Boya Molu.

Hata hivyo, tume hiyo inasema kuwa imeweza kuendesha chaguzi kadhaa ndogo tangu wakati huo, shughuli ambazo zilihusisha utoaji wa “maamuzi yenye uzito kikatiba”.

You can share this post!

TSC yaadhibu walimu wanaotoza karo zaidi

Wabunge wakataa pendekezo la kupunguza riba ya mikopo ya...