IEBC: Sonko yuko huru kuwania kiti kwa sasa

IEBC: Sonko yuko huru kuwania kiti kwa sasa

VALENTINE OBARA NA KENNEDY KIMANTHI

GAVANA wa zamani wa Nairobi, Bw Mike Sonko (pichani), atakuwa huru kisheria kuwania ugavana Mombasa mradi tu awe amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa bunge la kaunti ya Nairobi kumtimua mamlakani.

Haya yamethibitishwa baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufafanua kuwa, haina mamlaka ya kuzuia mwanasiasa yeyote aliyekata rufaa kwa kubanduliwa mamlakani asiwanie tena kiti cha kisiasa.

Kamishna wa IEBC, Prof Abdi Guliye, Jumatatu alisema tume hiyo haina budi ila kufuata sheria jinsi ilivyo kuhusu suala hilo ambalo linagusia pia aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu.

“Sheria inasema kuwa, kama mahakama imeamua ulitolewa mamlakani kihalali kwa sababu ya makosa fulani uliyotenda katika utekelezaji wa majukumu yako, lakini kuna rufaa ulizowasilisha dhidi ya maamuzi hayo, basi una haki ya kuwania kiti cha kisiasa. Lakini iwapo utakuwa umekamilisha rufaa zote na uamuzi wa mwisho haujapingwa, basi hapo ndipo hufai kuwania,” akasema Prof Guliye, katika mahojiano ya runinga.

Bw Sonko alibanduliwa na Bunge la Kaunti ya Nairobi mnamo Desemba 3, 2020, kwa madai mbalimbali ikiwemo utumizi mbaya wa fedha za umma na ukiukaji wa Sura ya Sita ya Katiba kuhusu uadilifu.

Seneti ilipiga kura kuidhinisha uamuzi wa bunge la kaunti mnamo Desemba 17, 2020.

Mnamo Machi, Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu ambayo ilishikilia kwamba, Bw Sonko aliondolewa mamlakani kisheria, kinyume na madai yake kuwa sheria zilikiukwa na hakutendewa haki.

Alielekea katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi huo, na sasa IEBC imefafanua haiwezi kumzuia kuwania hadi rufaa yake ikamilike na iwapo hataibua malalamishi mengine tena mahakamani kuhusu suala hilo.

Mwanasiasa huyo ameshikilia kuwa kutolewa kwake mamlakani kulichochewa kisiasa na atazidi kujitetea hadi atakapoondolewa lawama.

Bw Sonko alizindua rasmi kampeni zake za kuwania ugavana Mombasa ifikapo Agosti, wikendi iliyopita.

Amepangiwa kuwania kiti hicho kupitia Chama cha Wiper kinachoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais, Bw Kalonzo Musyoka.

Hivi majuzi, Bw Musyoka, ambaye ni wakili alisema anafahamu vyema sheria haiwezi kumzuia Bw Sonko kuwania ugavana kwa sasa.

Uamuzi wake kuwania wadhifa huo umevutia hisia kali baina ya viongozi mbalimbali wa Mombasa wanaompinga, akiwemo Gavana Hassan Joho, Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, na aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo, Bw Hassan Omar.

Bw Nassir ndiye mgombeaji wa ugavana kupitia kwa ODM, naye Bw Omar akiwa mgombeaji kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Mojawapo ya pingamizi lao dhidi ya Bw Sonko ni kuwa, kubanduliwa kwake mamlakani alipokuwa gavana Nairobi kulithibitisha yeye si mwadilifu na hivyo basi hastahili kupewa nafasi ya kusimamia Kaunti ya Mombasa.

Kesi nyingine iliyowasilishwa mahakamani Mombasa kumzuia kuwania ugavana bado inasubiriwa kukamilika.

Kwa upande wake, Bw Waititu alikuwa akilenga tikiti ya UDA kuwania ugavana Kiambu lakini akashindwa na Seneta Kimani Wamatangi.

Bw Waititu hajaamua hatua atakayochukua baada ya hapo.

Licha ya hayo, Prof Guliye alisema makamishna wa IEBC bado watakutana kujadili suala hilo tata linalohusu magavana walioondolewa mamlakani ambao wanataka kuchaguliwa tena, kabla uamuzi wa mwisho utangazwe rasmi.

Mbali na magavana waliotimuliwa mamlakani ambao wanataka kuwania viti katika uchaguzi ujao, kumekuwa pia na mjadala kuhusu wawaniaji wa viti vingine ambao wana kesi mahakamani.

Idadi kubwa ya wabunge na maseneta wanaandamwa na kesi mbalimbali zikiwemo za madai ya ufisadi, uchochezi wa ghasia na mauaji lakini kisheria, watakubaliwa kuwania viti vya kisiasa kwa vile hawajahukumiwa na wengine walikata rufaa dhidi ya hukumu zao.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool kigezoni dhidi ya Aston Villa

Maskwota Lamu watishia kususia uchaguzi mkuu

T L