IEBC yaita wawaniaji Jumatano

IEBC yaita wawaniaji Jumatano

NA CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewaalika wagombea urais wote wanne kwa mkutano wa kujadili masuala mbalimbali kuhusu sajili ya wapigakura.

Mwaliko wa mkutano huo, utakaofanyika Juni 29, 2022, katika mkahawa wa Windsor, unajiri wakati ambapo malalamishi yametokea kufuatia tangazo la IEBC kwamba sajili ya kidijitali pekee ndiyo itatumika kuwatambua wapigakura Agosti 9.

Katika barua iliyotumwa kwa wagombea urais Naibu Rais William Ruto (Kenya Kwanza), Raila Odinga (Azimio) Profesa George Wajackoyah (chama cha Roots) na David Mwaure Waihiga (Chama cha Agano) IEBC inapendekeza kuwa kila mmoja wao ataruhusiwa kuandamana na wajumbe wasiozidi watano.

“Tume inakualika kwa mkutano wa mashauriano ya wagombeaji urais ambao umeratibiwa kufanyika mnamo Jumatano, Juni 29, 2022 katika mkahawa wa Windsor Golf and Country, Kiambu, kuanzia saa tatu asubuhi (9:00am),” ikasema barua hiyo.

IEBC imeorodhesha suala la sajili iliyochapishwa ya wapigakura, upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi na uoanishaji wa ratiba za kampeni za wagombea uchaguzi kama miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa.

“Tafadhali zingatia kuwa unaweza kuandamana katika mkutano huo na watu wasiozidi watano,” barua hiyo ikaamuru.

Bw Odinga amehoji hatua ya IEBC kuamuru kwamba sajili ya kidijitali pekee ndio itatumika kuwatambua wapiga kura na wala sio sajili mbadala wa daftari ni kinyume cha sheria za uchaguzi.

Kulingana na wakili wa mgombea urais huyo, Paul Mwangi, IEBC haitajatoa hakikisho yoyote kwa wagombeaji na Wakenya kwa ujumla kwamba mitambo yake ya kielektroniki (KIEMs kit) haitafeli.

Kulingana Bw Mwangi, IEBC inafaa kuruhusu matumizi ya sajili ya daftari kama mbinu mbadala ya kutambua wapigakura.

  • Tags

You can share this post!

Droo ya Dala Sevens yatangazwa, KCB na Strathmore kufufua...

13 wauawa polisi wakipambana na wahalifu Mexico

T L