Habari Mseto

IEBC yajitetea kuhusu matumizi ya Sh690m kwa mapochopocho

May 8th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumatano ilijitokeza na kujitetea kuhusu matumizi makubwa ya pesa kwa mapochopocho ya vyakula na vinywaji wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2017, ikilenga kujiondolea lawama.

Hii ni baada ya Mkaguzi Mkuu wa matumizi ya pesa za umma Edward Ouko kutoa ripoti kuwa tume hiyo ilitumia Sh691,526,310 kwa chakula wakati wa uchaguzi, ripoti ambayo ilivutia hisia kali kutoka kwa Wakenya.

Jana, IEBC ilituma ujumbe kufafanua jinsi pesa hizo zilitumiwa, ikitoa hesabu ya idadi ya wafanyakazi waliokuwa wakinunuliwa chakula hicho na kwa gharama gani.

“Idadi ya maafisa wa uchaguzi ilikuwa 469,712 na pesa zilizotumika ni Sh691,526,310, gharama ya wastani kwa kila mtu ilikuwa Sh1,472, kwa siku tatu na milo mara tatu kwa siku. Hivyo, kila mlo uligharimu Sh164, ama Sh491 kwa milo mitatu kwa siku,” IEBC ikasema kwenye akaunti yake ya Twitter jana.

Tume hiyo ilisema kuwa maafisa walionunuliwa vyakula wakati wa uchaguzi ni wasimamizi wa vituo, wasaidizi wao, makarani na maafisa wa usalama.

Tume hiyo imekuwa ikiingiliwa tangu Jumanne wakati ripoti ya Bw Ouko iliwekwa wazi, Wakenya wengi wakiikashifu kuwa ilitumia pesa za mlipa ushuru vibaya.