IEBC yakosa kutaja vituo visivyo na mfumo wa kisasa kutuma matokeo

IEBC yakosa kutaja vituo visivyo na mfumo wa kisasa kutuma matokeo

NA SAMWEL OWINO

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) bado imeweka siri taarifa kuhusu vituo 1,111 vya kupigia kura ambavyo havina mfumo wa kisasa wa mtandao wa 3G.

Ingawa tume hiyo ilitakiwa kuchapisha majina ya vituo hivyo na kueleza hatua iliyochukua kuboresha mtandao, Jumanne makamishna wa IEBC walisema suala hilo litajadiliwa tu na maajenti wa wanaowania urais.

“Tutawapeleka maajenti wa wanaowania urais kwenye bohari yetu na kuwaonyesha jinsi matokeo ya kura kutoka kwa vituo hivyo yatakuwa yakipeperushwa,” akasema Kamisha Abdi Guliye kwenye Ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Tume hiyo iliwaeleza wahariri wa vyombo vya habari kwamba tayari imenunua modemu za setilaiti zitakazosambazwa katika vituo hivyo 1,111 ambavyo havina mtandao wa 3G.

Mitambo hiyo ndiyo itakayotumiwa kupeperusha matokeo ya kura kuanzia jioni ya Agosti 9.

IEBC ilikuwa imependekeza kuwe na njia mbadala ya kupeperusha matokeo ya uchaguzi kupitia Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi, 2022, ili kushughulia hali ambapo kuna changamoto ya kuwasilisha matokeo.

Hata hivyo, pendekezo hili lilikataliwa bungeni.

Kifungu cha 39 cha Sheria za Uchaguzi kinalazimu maafisa wa IEBC watume matokeo ya kura za urais kupitia fomu 34A, itakayopigwa picha na kutumwa kielektroniki hadi kwa makao makuu ya eneo bunge pamoja na kituo cha kitaifa cha kujumlisha matokeo, kilichoko Bomas.

Mahakama ya Juu ilipobatilisha kuchaguliwa kwa Uhuru Kenyatta mwaka 2017, iliangazia matokeo kutoka vituo 11,000 vya kura katika maeneo ambayo kimsingi yanapaswa kuwa na mtandao mzuri wa intaneti.

Wakati huo, IEBC ilisema kwamba haikuweza kupeperusha matokeo kutokana na mtandao hafifu.

Upeperushaji wa matokeo ya kura hadi Kituo Kikuu cha Kujumlisha cha IEBC, kisheria hutakikana kiwe cha kielektroniki kutoka kwa kituo cha kupigia kura.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Commercial milk coolers husaidia kuhifadhi maziwa...

Msanii wa nyimbo za injili anayesaidia watoto mitaani

T L