IEBC yaonya Raila, Ruto kuhusu kampeni

IEBC yaonya Raila, Ruto kuhusu kampeni

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, amesema kampeni za mapema zinazoendeshwa na Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga ni haramu.

Vile vile, alisema kuanzia leo, Desemba 9, ni marufuku kwa wale wanaopania kuwania nyadhifa katika uchaguzi mkuu wa 2022, kushiriki katika hafla za kuchanga fedha, maarufu kama harambee.

Bw Chebukati alisema kampeni zinazoendesha na Dkt Ruto na Bw Odinga, sawa na zile zinazoendeshwa na vinara wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) zinakiuka sheria ya uchaguzi na “ni hatia kwa mujibu wa Sheria ya Uhalifu wa Uchaguzi ya 2016.”

Kwenye taarifa aliyotoa jana baada ya mkutano kati ya tume hiyo na Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) mjini Limuru, Bw Chebukati aliongeza kwamba, ni hatia kwao kuweka mabango maeneo mbalimbali nchini kujinadi.

“Kipindi cha kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022 hakijaanza. Izingatiwe kuwa kampeni huanza tu baada ya mtu kuidhinishwa na IEBC kushiriki uchaguzi”, Bw Chebukati akasema.“Kwa msingi wa maelezo hayo, yakiambatanishwa na sehemu ya 14 ya sheria ya uchaguzi, kampeni zinazoendelea sasa pamoja na kuwekwa kwa mabango ni hatia inayoweza kuvutia adhabu kwa mujibu wa sheria hiyo,” akaongeza bila kutaja adhabu yenyewe.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kipengele cha 13 cha Sheria ya Uhalifu wa Uchaguzi, atakayepatikana na hatia ya kuivunja atatozwa faini ya Sh500,000 au kifungo cha miaka mitano gerezani au adhabu zote mbili.Katika siku za hivi karibuni, Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakiendesha kampeni katika sehemu mbalimbali nchini katika jitihada za kuuza sera zao.

Naibu Rais amekuwa akiuza sera zake zinazojikita katika mpango wa uimarishaji uchumi wa walalahoi, almaarufu, “Bottom Up” huku Bw Odinga akiahidi kuwa, atatoa ruzuku ya Sh6,000 kila mweza kwa familia masikini chini ya kauli mbiu yake ya Azimio la Umoja.

Katika kampeni zake, Dkt Ruto amekuwa akitoa michango ya mamilioni ya fedha kupiga jeki biashara za makundi ya wahudumu wa boda boda na mama mboga miongoni mwa walalahoi wengine.Kesho jijini Nairobi, Bw Odinga anatarajiwa kutangaza rasmi kuwa atawania urais kwa mara ya tano 2022. Jumatano, azma yake ilipata uungwaji mkono kutoka kwa mabwanyenye kutoka Mlima Kenya.

Kampeni za Dkt Ruto na Odinga zimeonekana kukumbatiwa na idadi kubwa ya Wakenya kwani kutokana na matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na kampuni ya utafiti TIFA, wao ndio wagombeaji urais wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini.

Hali hii imekoleza dhana kuwa kinyang’anyiro cha urais 2022 kitakuwa mbio za ‘farasi’ wawili; Dkt Ruto na Bw Odinga. Hii ni licha ya kwamba, vinara wa OKA; Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Gideon Moi (Kanu) pia wametangaza nia ya kuwania urais na kupata idhini ya vyama vyao.

Lakini mnamo Novemba 22, Dkt Ruto alikanusha madai kwamba, ameanza kampeni za mapema za kusaka kura za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022. Akiongea na wanahabari katika makazi yake rasmi mitaani Karen, Nairobi, Dkt Ruto alisema ziara ambazo amekuwa akifanya maeneo mbalimbali nchini ni za kikagua miradi ya serikali.

“Sijaanza kampeni kwa sababu IEBC haijatangaza rasmi kipindi cha kampeni. Kile ninafanya ni wajibu wangu kama Naibu Rais. Hii ni kuwatembelea wananchi, kusikiza maoni yao na changamoto zao na kukagua miradi ya maendeleo kama vile barabara,” Dkt Ruto akaeleza.

Hata hivyo, hali halisi ni kwamba hakuna miradi ya serikali kuu ambayo Naibu Rais amewahi kukagua katika kampeni hizo ila amekuwa akiuza sera za chama cha United Democatic Alliance (UDA) .

You can share this post!

Kundi la wanakijiji tajiri lenye ushawishi mkubwa

Masonko waelezea sababu kuunga Raila kidole

T L