IEBC yatangaza chaguzi ndogo Bungoma na wadi tano nchini

IEBC yatangaza chaguzi ndogo Bungoma na wadi tano nchini

NA CHARLES WASONGA

KINYANG’ANYIRO cha kumrithi aliyekuwa Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kinatarajiwa kushika kasi kuanzia sasa.

Hii ni baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza kuwa uchaguzi huo utafanyika mnamo Desemba 8, 2022.

Kwenye ilani iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema kuwa amepokea barua kutoka Spika wa Seneti Amason Kingi alitangaza wazi wadhifa wa seneta wa Bungoma.

Hiyo ni kutokana na kujiuzulu kwa Bw Wetang’ula mnamo Agosti 19, 2022 kuwania wadhifa wa uspika wa Bunge la Kitaifa na akashinda.

“Kufuatia kutangazwa wazi kwa nafasi ya Seneta wa Kaunti ya Bungoma na kuthibitishwa na Spika wa Seneti kupitia barua niliyopokea mnamo Septemba 26, 2022 kutafanyika uchaguzi mdogo wa Seneta wa Bungoma mnamo Alhamisi, Desemba 8, 2022,” Bw Chebukati akasema.

Bw Wetang’ula alichaguliwa kwa muhula wa tatu kama seneta wa Bungoma katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Bw Chebukati alivishauri vyama vya kisiasa ambavyo vina nia ya kudhamini wagombeaji katika uchaguzi mdogo kufanya kura za mchujo kabla ya Oktoba 19, 2022.

“Vile vile, wale ambao wangependa kushiriki katika uchaguzi huo mdogo kama wagombeaji huru hawatahitajika kuwa wanachama wa vyama vya kisiasa angalau miezi mitatu kabla ya tarehe ya uchaguzi huo mdogo,” akasema Bw Chebukati.

Kando na uchaguzi mdogo wa useneta wa Bungoma, IEBC pia itaendesha chaguzi ndogo katika wadi za Ololmasani, Kyome/Thaana, Utawala, Mumias Kaskazini na Gem Kusini, katika kaunti za Narok, Kitui, Nairobi, Kakamega na Siaya, mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Maseneta wa Azimio wamkosoa Ruto kuhusu GMO

Ruto awasilisha bungeni majina ya watu 22 aliopendekeza...

T L