Habari Mseto

IEBC yatangaza upya nafasi ya Chiloba baada ya watu wachache kujitokeza

May 22nd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza upya nafasi iliyowazi ya Afisa Mkuu Mtendaji baadaya watu wachache kutuma maombi kufuatia tangazo la kwanza.

Kupitia tangazo la kulipiwa katika gazeti la Daily Nation, tume hiyo iliwashuri wale waliotuma maombi hapo awali kufanya hivyo kwa mara nyingine.

Siku ya mwisho ya barua za maombi kupokewa ni Jumatatu Juni 3, 2019.

Nafasi hiyo ilibaki wazi baada ya tume hiyo kumfuta kazi aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba ambaye alikuwa amesimamishwa kazi kuanzia Aprili 2018.

Bw Chiloba alifutwa kazi mnamo Septemba 24 mwaka jana baada ya kuelekezewa lawama katika ripoti ya ukaguzi wa ndani ya tume hiyo iliyofichua kuwa mamilioni ya pesa za umma yalipotezwa katika ununuzi wa bidhaa na huduma kinyume cha sheria kwa ajili ya kuendesha uchaguzi mkuu wa 2017.

Mnamo Machi mwaka huu Jaji wa Mahakama ya Leba Hellen Wasilwa alitoa uamuzi wa muda wa kusitisha uajiri wa afisa mkuu mwingine kufuatia ombi lililowasilishwa na Henry Mutundu aliyepinga mchakato huo.

Matundu alidai kuwa utaratibu uliotumiwa kuajiri afisa mkuu mpya ulikiuka Katiba kwani haukuzingati uwazi, haki na uwajibikaji unavyohitajika.

Wakati huu, IEBC inaendesha shughuli zake ikiwa na makamishna watu pekee; ambao ni mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishna Boya Molu na Profeasa Abdi Guliye.

Baada ya tume hiyo kumwamuru Bw Chiloba kwenda likizo ya lazima mnamo Aprili 12, 2018, makamishna Connie Maina, Paul Kurgat na Margret Mwachanya Wanjala walijiuzulu mnamo Aprili 16, 2018.