IEBC yathibitisha kupokea sahihi za kutaka serikali ya Taita Taveta ivunjwe

IEBC yathibitisha kupokea sahihi za kutaka serikali ya Taita Taveta ivunjwe

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imethibitisha kwamba imepokea sahihi 52,000 za watu wanaopendekeza kuvunjwa kwa serikali ya Kaunti ya Taita Taveta.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati amesema Jumatano kwamba maafisa wake watazikagua sahihi hizo kwa muda wa siku tano zijazo ili kubainisha ikiwa ni halali au la.

“Leo (Jumatano) tumepokea rasmi ombi la Gavana wa Taita Taveta la kutaka kaunti hiyo ivunjwe. Tutazikagua sahihi zote 52,000 zilizoandamanishwa nayo kubaini ikiwa ni hali kabla ya kutoa mwelekeo,” Chebukati akasema Jumatano ofisini mwake katika makao makuu ya tume hiyo katika jumba la Anniversary, Nairobi.

Ikiwa IEBC itaridhika kuwa sahihi hizo ni sahihi, Gavana Samboja ataweza kupawasilisha ombi hilo kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa uchunguzi zaidi.

Na ikiwa Rais ataridhishwa na masuala yaliyoibuliwa katika ombi hilo, atabuni jopo ambalo litachunguza suala hilo na kutoa mapendekezo yake.

Hatua hii ya Bw Samboja kutaka kuvunja serikali ya Kaunti ya Taita Taveta ni mojawapo ya sababu zilizochangia madiwani wa kaunti hiyo kutaka kumwondoa ofisini.

Hata hivyo, jaribio lao lilizimwa na bunge la seneti lililodai madai yao hayakuwa na mantiki.

You can share this post!

Sarah Cohen ataka achukue nguo katika makazi yanayotajwa...

Afueni kwa serikali za kaunti baada ya Kemsa kukubali...

adminleo