Makala

Ielewe teknolojia ya kisasa ya kuotesha mbegu

November 13th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

Mafanikio katika shughuli za kilimo-biashara yanaegemea mambo kadha wa kadha, ambayo mkulima anapaswa kutilia maanani ili kuyaafikia.

Kando na kujihami na utafiti wa kutosha kujua anachofaa kukuza na ni eneo lipi bora, ikiwa ni pamoja na kuwa na soko tayari la mazao, uhalisia wa pembejeo yaani mbegu, mbolea na dawa, unatajwa kama mojawapo ya nguzo kuu kufanikisha kilimo.

Pembejeo bandia na ambazo hazijaafikia ubora wa bidhaa, ni miongoni mwa changamoto zinazozingira wakulima, na zimechangia kwa kiwango kikubwa kulemaza azma yao.

Katika eneo tulivu la Kennol, Kaunti ya Murang’a, wanandoa wawili wachanga wamejituma kuangazia baadhi ya masaibu yanayofika wakulima.

Lamech Kabuti, 25, na mchumba wake Loise Ndung’u, 21, wanafanya kilimo cha kuotesha mbegu kupata miche ya mimea mbalimbali.

Unapozuru eneo hilo, utalakiwa na rangi ya kijani cha matunda kama vile maembe, maparachichi, mapapai, karakara na ndizi. Pia kuna wanaokuza mahindi na maharagwe.

Katika shamba la familia ya wanandoa hao lenye ukubwa wa ekari nne, ingawa taswira inawiana na ya mazingira jirani, kuna suala moja tu linalowafanya kuwa wa kipekee. Kwenye mgunda huo, wana kivungulio ambacho kwa upeo wa macho utadhani kinatumika kuzalisha nyanya, pilipili mboga au mazao mengine yanayolimwa kwenye mahema.

Loise Ndung’u, meneja wa Victorious Green Farms akieleza kuhusu uoteshaji wa mbegu na miche kupitia mfumo wa kisasa wa trei. PICHA/ SAMMY WAWERU

Kikiwa na ukubwa wa mita 8, upana na urefu wa mita 40, kina shughuli maalum; ni kiunga cha kuotesha mbegu na miche.

Chini ya utambulisho Victorious Green Farms, kivungulio hicho kinaotesha miche ya nyanya, pilipili mboga za rangi mbalimbali wengi wanazitambua kama hoho, sukuma wiki, kabichi, broccoli na kolifulawa.

Aidha, kiunga hicho pia kinaotesha miche ya kupandikiza ya matunda mbalimbali kama vile maparachichi, maembe, machungwa na mapapai.

Lamech Kabuti, afisa mkuu mtendaji na mmwasisi wacho anasema huotesha mbegu za kabichi zenye asili ya Kichina. Kinyume na wanaootesha mbegu kwenye kitalu cha udongo, Victorious GreenFarms imekumbatia mfumo wa kisasa katika uzalishaji wa miche.

Kwenye kiunga cha wanandoa hao, wanatumia trei maalum zenye mashimo. “Aghalabu trei tunazotumia moja ina mashimo 200, japo kuna za hadi mashimo 400,” Lamech na ambaye anajulikana kwa jina la lakabu kama Mkulima Mdogo adokeza.

Ukilinganisha na kitalu, mfumo huo unasifiwa kwa kinachotajwa kama “kufanikisha uoteshaji na uchipukaji wa mbegu kwa takriban asilimia 100”.

Pili, miche inaepushwa dhidi ya changamoto za wadudu na magonjwa. “Miche inapooteshwa kwenye kitalu cha udongo eneo tambarare, huendelea kusambaza magonjwa na wadudu inapohamishiwa shambani. Mfumo tuliokumbatia unapunguza kwa kiasi kikubwa athari hizo,” anaelezea Loise Ndung’u, meneja Victorious Green Farms.

Trei maalum kuotesha mbegu. Mfumo wa trei ni nafuu pamoja kuwa salama kwa mbegu na miche. Picha/ SAMMY WAWERU.

Isitoshe, kwa kutumia trei na kwenye kivungulio, Loise anasema miche inaondolewa ‘msongo wa mawazo’ unaosababishwa na miale kali ya jua. “Chini ya mfumo wa kisasa, miche inakuwa salama jambo linalochangia kuongezeka kwa kiwango cha mazao,” asisitiza.

Fauka ya tija hizo, miche inachukua muda mfupi kuwa tayari kwa upanzi.

Lamech anasema miche inayochukua kati ya wiki 5 – 7, kwa kutumia trei muda huo unapungua hadi wiki 4 au 5. Akitoa mfano wa Uholanzi, anasema kinachofanya nchi hiyo kuimarika katika sekta ya kilimo ni anachotaja kama kukumbatia mfumo huo wa kisasa katika kuotesha mbegu.

Kivungulioni, trei wamezitengenezea meza maalum zilizoinuliwa futi kadhaa juu, wakizitambua kama ‘beds’.

Kimsingi, wataalamu wanasifia matumizi ya trei kuotesha mbegu wakihoji zinapunguza gharama. “Kwa kutumia trei, una uhakika mbegu zitaota kwa karibu asilimia 100 kwa 100. Ni mfumo ambao unapunguza gharama, ikikumbukwa kwamba athari za wadudu na magonjwa zinaepukwa,” anafafanua Lawrence Ngugi, mtaalamu wa kilimo kutoka Hygrotech, kampuni ya uzalishaji na uoteshaji mbegu iliyoko Naivasha.

Victorious Green Farms inazingatia uzalishaji wa miche kwa njia asilia. Lamech akidokeza kwamba hawatumii fatalaiza wala kemikali yoyote.

“Badala ya udongo, tunatumia maganda ya nazi iliyokunwa, yakasagwa kisha yanatibiwa kwa dawahai. Watafiti wa masuala ya kilimo na asasi husika wamethibitisha kuwa maganda hayo ni salama,” akasema wakati wa mahojiano.

Muhimu zaidi katika kuotesha miche kupitia mfumo huo, ni kuzingatia kiwango cha usafi, kiwe cha hadhi ya juu.

Wanaoingia kwenye kivungulio wanadhibitiwa, ambapo anayeruhusiwa sharti makanyagio yake ya viatu yatumbukizwe kwenye maji yaliyotibiwa kwa dawa na yaliyoko mlangoni.

Maji yanayotumika kunyunyizia miche, Lamech anasema lazima yawe safi na wana bwawa ndogo linalowasambazia kiungo hicho. PICHA/ SAMMY WAWERU

Safari ya Victorious Green Farms ilianza 2016, Lamech akifichua kwamba hiyo ni baada ya kuhusika katika ajali mbaya na ambapo alilazwa hospitalini muda wa mwaka mmoja mfululizo.

“Hospitalini, matunda niliyopendekezewa nile kama vile karakara, matundadamu na mapapai yalikuwa nadra kupatikana,” anaeleza.

Kulingana na maelezo yake, alipopata nafuu, changamoto alizopitia – ukosefu wa matunda, zilimchochea kuingilia shughuli za uoteshaji mbegu na miche ya miti ya matunda.

Anafichua kwamba alianza kwa mtaji wa Sh10, 000 pekee na ni kupitia oda za wateja wake alipata wazo la kuotesha miche ya nyanya, pilipili mboga za rangi tofauti, sukuma wiki, kabichi, broccoli na kolifulawa.

Anasema uwekezaji katika kivungulio, ulimgharimu kima cha Sh140, 000.

Akikadiria gharama ya kuotesha mche mmoja kuwa kati ya Sh1 – 2, anasema Victorious Green Farms kwa mwezi hufanya mauzo ya miche isiyopungua 40, 000.

Huuza mche mmoja kati ya Sh2 – 15, huku akitumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na WhatsApp kutafuta soko.