Makala

IGAD: Je, Kalonzo amekataliwa kuongoza tume ya amani?

January 7th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HALI ya wasiwasi imegubika utendakazi wa aliyekuwa Naibu Rais Kalonzo kama Msimamizi wa Tume ya Pamoja ya Kusimamia Amani (JMEC) nchini Sudan Kusini baada ya mataifa wanachama wa Shirika la Maendeleo la IGAD kuchelewa kuidhinisha uteuzi wake.

Bw Kalonzo aliteuliwa na Kenya kuongoza tume hiyo mnamo Novemba 2018 lakini hali ya kutoelewana imeibuka kuhusu uteuzi wake.

Duru katika ngazi za kidiplomasia zinasema kuwa wadau wengine katika mzozo nchini Sudan Kusini wanapinga uteuzi huo. Vile vile, hawataki Kenya na wanachama wengine wa IGAD kuongoza mchakato huo wa amani.

Bw Musyoka, ambaye ni kiongozi wa chama cha Wiper alitarajiwa kuchukua mahala pa aliyekuwa Rais wa Bostwana Festus Mogae ambaye alijiuzulu wadhifa huo Agosti mwaka 2018.

Tayari Serikali ya Kenya imewasilisha jina la Bw Musyoka kwa IGAD ambayo ndio itasimamia utendakazi wa JMEC, ili iidhinishwe, duru zilisema

Lakini afisa mmoja wa ngazi ya juu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni, ambaye aliomba jina lake linabwe, alisema uteuzi wa Kalonzo haujafutiliwa mbali lakini unasibiri uidhinishwaji kutoka kwa mataifa wanachama wa IGAD.

“Tunafahamu kuhusu uvumi unaoenea kwamba uteuzi wake umekataliwa. Ukweli ni kwamba Kenya iliwasilisha jina lake na inasubiri kikao cha viongozi wa mataifa wanachama wa IGAD kumwidhinisha,” akasema afisa huyo.

Wakati wa msimu wa Krismasi Bw Musyoka alisafiri hadi Sudan Kusini ambapo alikutana na Rais Salva Kiir.

Inadaiwa kuwa upande mmoja katika mzozo wa Sudan Kusini, unaongozwa na kiongozi wa waasi, Riek Machar, haujachangamkia uteuzi wa Bw Musyoka, ambaye wanamsawiri kama mwandani wa chama tawala, SPLA.

Viongozi wa mrengo huo wanasema Bw Musyoka amewahi kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa SPLA alipohudumu kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kenya katika miaka ya 1990s.

Uteuzi wa Bw Musyoka ulijiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuridhiana na kiongozi wa upinzani, NASA, Raila Odinga mnamo Machi 9, 2018. Ni katika moyo huo wa kupalilia maridhiano ya nchini ambapo Rais Kenyatta aliamua kumkumbatia kiongozi huyo wa chama cha Wiper.

Wa kwanza kufaidi kutokana na maridhiano hayo ni Bw Odinga ambaye Rais Kenyatta alitumia ushawishi wake na kumwezesha kuteuliwa kama Balozi Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundo Msingi.

Kabla ya uteuzi wake, Bw Musyoka alitangaza hadharani kwamba yuko tayari kuwa “mtu wa mkono” wa Rais Kenyatta. Alitoa tangazo hilo katika mazishi ya babake katika eneo bunge la Mwingi Kaskazini mnamo Septemba, 2018.

Hata kabla ya uteuzi wake kurasimishwa, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kenya Dkt Monic Juma alimwasilisha Bw Musyoka kwa Rais Kiir mnamo Novemba, 2018.

Vile vile, inadaiwa kuwa wanachama wa IGAD hawakufurahishwa na uteuzi huo kwa sababu ulifanywa bila wao kushauriwa.

“Hakukuwa na mashauriano kati ya Kenya na mataifa wanachama wa IGAD kabla ya Kalonzo kuteuliwa. Marais wa mataifa hayo walichukulia uteuzi huo kama dharau au matusi kwao,” afisa mmoja kutokana taifa moja wanachama wa IGAD alisema.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Kenya ndiyo inalaumiwa kwa mzozo huo wa kidiplomasi, kwa kutozingatia masuala kadha muhimu kabla ya jina la Bw Musyoka kuwasilishwa mbele ya kikao cha Marais wanachama wa IGAD.

“Taratibu na itifaki ya uteuzi na uidhinishwaji wa balozi maalum hazikufuatwa na ndio maana IGAD imekataa kuidhinisha uteuzi wake,” afisa huyo akaeleza.

Awali, inadaiwa kuwa Kikao cha Marais wa Mataifa wanachama wa IGAD kilikuwa kimependekeza kuwa mwenyekiti wa tume ya JMEC angalau awe rais wa zamani.

Kikao hicho pi kilitaka mwenyekiti huyo ateuliwe kutoka taifa lisiloegemea upande wowote katika mzozo wa Sudan Kusini.

Hii ina maana kuwa mtu kutoka mataifa kama vile, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia, Eritrea na Somalia hangefaa kuteuliwa katika wadhifa huo kwa sababu ni majirani za Sudan Kusini.

JMEC ilibuniwa mahsusi kusimamia utekelezaji wa mkataba wa Amani uliotiwa saini na Rais Kirr na mpinzani wake mkuu Bw Machar mwaka jana.