Michezo

Ighalo ashangazwa na mazoezi chini ya masharti mapya

June 11th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MSHAMBULIAJI Odion Ighalo wa Manchester United amesema mazoezi anayofanya kwa sasa ni mapya kabisa katika maisha yake ya soka.

United kama ilivyo timu zingine za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ilirejea mazoezini kujiandaa kwa marejea ya michuano ya ligi hiyo, lakini chini ya vikwazo vikali vya afya.

“Kwa hakika, ni mazoezi ya ajabu, kwa sababu lazima ukae umbali wa mita mbili na mwenzako, hata kuongea lazima useme kwa sauti ya juu,” alisema kupitia kwa mtandao.

“Wakati mwingine inabidi uonyeshe kwa ishara, wakati mwenzako ako mbali, kwa kweli ni mazoezi mapya kwa kila mtu.”

Hata hivyo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 amedai kwamba wachezaji wote wamefurahia mazoezi hayo kuliko walivyokuwa wakijinoa kivyao manyumbani mwao kutokana na janga la corona.

“Kila mtu lazima ashiriki ili ajiweke katika hali nzuri. Kila mtu anaonekana kuyafurahia. Kukimbia, kujitahidi, na kupiga mpira, kupepetan mpira na kadhalika ni baadhi ya vitu tunavyofanya uwanjani.”

Ighalo alieleza furaha yake kufuatia kurejea kwa Pual Pogba na Marcus Rashford, wakati timu hiyo inajiandaa kukutana na Tottenham Hotspur mnamo Juni 19.

“Kila mtu anajiandaa vyema tayari kwa mechi ijayo. Kila mtu amerejea. Hata Paul amerudi katika hali yake bora. Kila mtu anajiandaa kama kawaida. Kikosi kwa sasa kipo imara, na kila mtu yuko tayari,” aliongeza Ighalo.