Michezo

Ighalo kuondoka Manchester United na kurejea kwa waajiri wake Shenhua

May 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MFUMAJI Odion Ighalo, 30, anatarajiwa kubanduka Manchester United wiki hii baada ya waajiri wake Shanghai Shenhua kufichua kwamba wanamhitaji kwa minajili ya kampeni za Ligi Kuu ya China.

Fowadi huyo mzawa wa Nigeria alijiunga na Man-United mnamo Januari 2020 mkopo ambao ungemshuhudia akiwajibishwa ugani Old Trafford hadi mwisho wa msimu huu; yaani Mei 30.

Kuahirishwa kwa kampeni za soka msimu huu kutokana na janga la corona kumeshuhudia vikosi vyote vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) vikirefusha kwa muda mikataba ya wachezaji ambao kandarasi zao zilikuwa zikitamatika hivi karibuni.

Ingawa yalikuwa matarajio ya Man-United kuendelea kujivunia huduma za Ighalo hadi baada ya mechi zote zilizosalia katika EPL msimu huu kusakatwa, mpangilio huo hautawezekana kwa sasa kwa kuwa Shenhua wanamtaka sogora huyo awe sehemu ya kikosi chao kinachoanza kujiandaa kwa marejeo ya Ligi Kuu ya China (CSL) wiki ijayo.

Ingawa hakuna tarehe mahsusi ambayo imetolewa kwa kivumbi cha CSL kurejelewa, Shenhua wanahisi kwamba Ighalo ni sehemu muhimu zaidi katika maandalizi yao.

Kubwa zaidi katika matamanio ya Ighalo lilikua ni kusalia ugani Old Trafford kwa matumaini kwamba kocha Ole Gunnar Solskjaer angeshawishi usimamizi wa Man-United kumpokeza mkataba wa kudumu baada ya kuafikia na Shenhua.

Japo ujio wa Ighalo kambini mwa Man-United ulikashifiwa, mchango wake kambini mwa miamba hao wa soka ya Uingereza umekuwa mkubwa baada ya kufunga mabao manne kutokana na mechi tatu alizopiga.

Kupona kwa Marcus Rashford kunadidimiza zaidi matumaini ya Ighalo kuendelea kuhudumu kambini mwa Man-United ambao kwa sasa wanapania kusajili washambuliaji wengine chipukizi watakaowasaidia kufikia maazimio yao ya baadaye.