Iheanacho atokea benchi na kuokoa chombo cha Leicester City dhidi ya Brighton kwenye Kombe la FA

Iheanacho atokea benchi na kuokoa chombo cha Leicester City dhidi ya Brighton kwenye Kombe la FA

Na MASHIRIKA

KELECHI Iheanacho alifunga bao katika sekunde za mwisho wa kipindi cha pili na kuwasaidia Leicester City kufuzu kwa robo-fainali za Kombe la FA msimu huu baada ya kuwapiga Brighton 1-0 mnamo Jumatano usiku ugani King Power.

Goli hilo la Iheanacho aliyetokea benchi katika kipindi cha pili, lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo Youri Tielemans.

Baada ya makocha wa timu zote mbili kufanyia vikosi walivyotegemea katika michuano ya awali mabadiliko saba, kipindi cha kwanza kilishuhudia kila mmoja akicheza kwa tahadhari kubwa.

Ilikuwa hadi kipindi cha pili ambapo kila timu ilianza kushambulia na bao la Andi Zeqiri kwa upande wa Brighton na la Cengiz Under kwa upande wa Leicester yakafutiliwa mbali kwa madai kwamba yalifumwa wavuni wawili hao wakiwa wameotea.

Droo ya robo-fainali ya Kombe la FA msimu huu itafanyika leo Alhamisi ya Februari 11 huku mechi hizo za hatua ya nane-bora zikitarajiwa kupigwa wikendi ya Machi 20-21.

Chini ya mkufunzi Brendan Rodgers, Leicester kwa sasa wamepoteza mchuano mmoja pekee kati ya 13 iliyopita na wamefuzu kwa robo-fainali za Kombe la FA mara mbili mfululizo. Ufanisi huo ni wao wa kwanza tangu 1968-69.

Afueni kubwa zaidi kwa Leicester ni kupona kwa mwanasoka James Justin ambaye kocha Rodgers amesema atakuwa na mchango mkubwa katika maazimio yao ya kutia kapuni angalau taji moja msimu huu.

Bao la Iheanacho lilikuwa lake la tano kufikia sasa msimu huu na alilifunga dakika chache baada ya Adam Lallana wa Brighton kukosa fursa nzuri ya kumwacha hoi kipa chaguo la pili kambini mwa Leicester, Danny Ward.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Brighton kupoteza mechi dhidi ya Leicester kwenye mapambano ya kuwania makombe mbalimbali. Awali, Brighton walikuwa wamewadengua Leicester mara tatu kwenye Kombe la FA na League Cup.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Atalanta yadengua Napoli na kujikatia tiketi ya kuvaana na...

Fowadi Moise Kean awabeba PSG hadi ndani ya 32-bora French...