HabariSiasa

Iko wapi elimu ya bwerere?

January 17th, 2020 3 min read

Na WAANDISHI WETU

IDADI kubwa ya watoto waliofanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka uliopita hawajaripoti shule walizoitwa kwa kukosa karo.

Hali hii imeibua maswali kuhusu jinsi misaada ya kifedha kwa masomo (basari) hupeanwa na pia uhalisia wa ahadi ya Serikali ya elimu bila malipo.

Mamilioni ya pesa kutoka serikali kuu, kaunti na maeneobunge hutengwa kila mwaka kwa minajili ya utoaji basari hasa kwa wanafunzi werevu wanaotoka katika familia zisizojiweza kifedha.

Kando na haya, kuna mashirika mengi ya kibinafsi yakiwemo mabenki ambayo hutoa ufadhili wa masomo.

Leo ikiwa ni siku ya mwisho kwa wanafunzi walioitwa kujiunga na shule za upili za kitaifa kwenda shuleni, Taifa Leo imebainisha bado kuna wengi ambao bado wako manyumbani.

Mmoja wao ni Isaac Keith, 13, aliyepata alama 406 lakini hana uwezo wa kulipa karo ya shule ya upili ya St Joseph’s Kitale ambako aliitwa.

Alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Roots mtaani Pipeline, eneo bunge la Gilgil katika Kaunti ya Nakuru na akaibuka mwanafunzi wa tano bora kati ya wanafunzi 165 katika KCPE.

“Alitakiwa kuripoti Jumatano lakini nimekosa karo. Nimejaribu kila niwezalo lakini sijapata usaidizi,” akasema mamake, Bi Lydia Kerubo.

Alieleza kwamba mwanawe alipata ufadhili wa miaka minne katika shule ya msingi ambayo ilimlipia karo hadi akakamilisha darasa la nane.

Juhudi za kutafuta uhisani kutoka kwa Wings To Fly ya Benki ya Equity, benki ya KCB na pia serikali ya kaunti hazijafua dafu.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, Mike Ngugi kutoka kijiji cha Thiiti ambaye alipata alama 417 katika KCPE anahofia kutojiunga na Shule ya Meru School alikoitwa.

Babake, Bw Albert Mati, ambaye ni bawabu, alisema amefanikiwa tu kupata Sh8,000 kupitia kwa misaada ya jamaa zake na Sh16,000 kutoka kwa hazina ya eneobunge, ilhali karo pamoja na sare ya shule ni Sh51,216.

“Katika shule ninakofanya kazi, nilikubaliana na wasimamizi kuwa mshahara wangu utumiwe kulipia karo ya binti yangu kwani sina namna nyingine,” akasema.

Mike alihitajika kujiunga na shule hiyo ya upili Jumatatu, Januari 13.

Hali sawa na hii inamkumba Philip Amuma Lukas kutoka Kaunti ya Tana River. Alipata alama 320, akaitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Nyambaria.

Mamake, Bi Josephine Falama ambaye ni kibarua katika serikali ya kaunti hupokea Sh4,700 pekee kila mwezi. Lukas anahitaji zaidi ya Sh53,000 kwa karo na mahitaji mengine ya shule.

“Cha muhimu kwangu kwa sasa ni masomo ya wanangu. Maombi yangi sio ya utajiri bali wanangu wapate karo wasome. Nina imani ombi langu litatimia,” akaeleza.

Kelvin Otieno alitakikana kujiunga na Shule ya Upili ya St Mary’s Yala, Kaunti ya Siaya baada ya kupata alama 368 katika KCPE.

Mamake, Bi Judith Adhiambo alisema alifanikiwa kugharamia tu viatu vya mtoto wake, kwani yeye hufanya kibarua cha dobi.

“Nimejaribu kutafuta msaada kwa wanasiasa lakini wapi!” akasema.

Cynthia Ratemo, aliyepata alama 353 katika Shule ya Msingi ya Soko, eneobunge la Kitutu Chache Kusini, Kaunti ya Kisii, ameshidnwa kigharamia zaidi ya Sh43,000 zinazohitajika kujiunga na Shule ya Upili ya St Charles Lwanga Ichuni.

Mlezi wake ni nyanyake, kwani babake alifariki alipokuwa na umri wa miaka miwili kisha mamake akaenda kuolewa kwingine.

Katika eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya, Trizer Martah aliyepata alama 343 katika KCPE huenda akakosa kujiunga na Shule ya Upili ya St Augustine Nyamonye alikoitwa.

Leonard Kipkorir Langat alipata alama 360 katika Shule ya Msingi ya Olgos Sopia, Kaunti ya Narok akaitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Kericho lakini angali nyumbani.

Pauline Gati, 14, huenda akakosa kuendeleza masomo yake katika Shule ya Upili ya St Clare Kioge baada ya kupata alama 308 katika KCPE.

Jumatatu aliandamana na mamake hadi katika shule hiyo bila chochote akiwa amevaa sare za shule ya msingi aliyosomea, lakini naibu mwalimu mkuu Frank Osoro akawashauri warejee baadaye wakiwa na angalau bidhaa chache muhimu atakazohitaji shuleni.

Naye Nyarangi Obed Onyancha amegeuka mtoto wa kurandaranda mitaani katika Kaunti ya Kisii. Alipata alama 220 katika KCPE ndipo akaanza kuishi mitaani tangu Desemba kwani mamake alimwambia hakuna matumaini kuendeleza masomo.

Alikuwa ameitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Bobaracho iliyo Kaunti ya Kisii.

Beckalm Kegesa ni yatima. Alifanikiwa kupata alama 246 katika Shule ya Msingi ya Mercy Academy iliyo Kisii alipopata ufadhili. Sasa anatakikana ajiunge na Shule ya Upili ya Nyamagwa, lakini nyanyake, 72, ambaye ndiye mlezi wake, amelemewa kifedha.

Shantel Nyaboke aliyefanya KCPE katika Shule ya Msingi ya Mama Ngina, Kaunti ya Nakuru alipata alama 239 akaitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Uhuru. Mamake, Bi Ruth Machoki, anasema haoni kama hilo litawezekana kwani hana namna kifedha.

Ripoti za SHARON ACHIENG, PHYLLIS MUSASIA, ALEX NJERU, STEPHEN ODUOR, JOSEPH OPENDA, RUTH MBULA, DICKENS WASONGA NA BENSON AYIENDA