Habari za Kitaifa

Iko wapi gesi ya Sh500? Kilio mtungi wa kilo 13 ukiongezeka hadi Sh3,231

April 3rd, 2024 1 min read

KABUI MWANGI NA WANDERI KAMAU

BEI ya gesi ya kupikia iliongezeka na kufikia Sh3, 231 kwa mtungi wa kilo 13 mnamo Machi, mwelekeo ambao ni kinyume na mpango wa serikali kupunguza bei za bidhaa hiyo, ikiwemo uondoaji wa ushuru wa asilimia nane.

Takwimu kutoka kwa Halmashauri ya Kitaifa ya Kukusanya Takwimu (KNBS), zilionyesha kuwa bei za wastani za bidhaa hiyo ziliendelea kuongezeka mwezi huo, kwa asilimia 1.4.

Hilo ni ikilinganishwa Februari, ambapo bei ya wastani ya bidhaa hiyo ilikuwa Sh3, 187.

Bei hiyo mpya ya wastani ni ya juu ikilinganishwa na Juni 2022, ambapo bei ya bidhaa hiyo ilifikia Sh3,218 kutokana na mzozo uliotokana na mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea baina ya Urusi na Ukraine.

Mnamo Jumatatu, uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa bei ya kujaza mtungi wa kilo 13 ilikuwa Sh3,330 katika baadhi ya maduka. Hilo ni ikilinganishwa na bei ya wastani ya kitaifa, ambayo ni Sh3,090.

Kulingana na wadadisi, ongezeko hilo limechangiwa na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu nyingine za kigeni.

“Ninaamini kuwa hili limechangiwa na kushuka kwa thamani ya shilingi, kama ilivyoshuhudiwa mwishoni mwa 2023 na mwanzoni mwa mwaka huu,” akasema mwenyekiti wa Chama cha Wauzaji Bidhaa za Mafuta Kenya (POAK), Bw Martin Chomba.

“Bei za gesi katika kiwango cha kimataifa zilipanda kutokana na hali ilivyo nchini Urusi. Hata hivyo, naona hali ambapo huenda bei hizo zikaanza kushuka katika siku za hivi karibuni kutokana na kuimarika kwa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni katika majuma kadhaa yaliyopita,” akasema.

Mwaka uliopita, serikali iliondoa ushuru wa asilimia nane ambao ulikuwa ukitozwa bidhaa hiyo ili kupunguza bei zake, ijapokuwa hilo halijaonekana kuwaletea Wakenya afueni yoyote.