Habari Mseto

Ikulu yaingilia kati mzozo wa KQ

October 24th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

IKULU ya Nairobi imeingilia kati mzozo wa Shirika la Ndege la KQ kuhusu ziara ya kwanza ya moja kwa moja Marekani.

Ikulu iliamrisha KQ kusuluhisha mzozo huo mara moja kwa lengo la kuhakikisha kuwa ziara ya moja kwa moja Jumapili Oktoba 28, 2018.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena alisema afisi ya Rais ilikuwa na hofu kuhusiana na mzozo huo kati ya wafanyikazi na usimamizi wa Kenya Airways.  Kulingana naye, Ikulu ilitaka kuhakikishiwa kuwa mzozo huo utasuluhishwa kabla ya ziara hiyo.

“Kenya Airways imetuhakikishia kuwa ziara ipo,” alisema Bi Dena.

Alisema hayo huku Wizara ya Uchukuzi ikiwa pia imeingilia kati mzozo huo na tofauti kati ya chama cha wahudumu wa shirika hilo na usimamizi wake.

Waziri wa uchukuli James Macharia alisema wakati wa mahojiano kwamba kutakuwa na maelewano na kuongeza kuwa wizara hiyo ilikuwa imezungumza na wakurugenzi wa bodi ya KQ ili waweze kusuluhisha mgogoro huo haraka iwezekanavyo.

Kulingana na Bw Macharia, bodi ya KQ inafaa kusikiza malalamishi ya wahudumu hao, “Hakunna mwajiriwa ambaye angependa kutishia mwajiri wake, hasa wakati mambo yanapoonekana kwenda shwari. Ikiwa KQ haitafaulu, ina maanisha kuwa washindani ndio watafaulu,” alisema.

Chama cha wahudumu kinataka wote watakaokuwa katika ziara hiyo kulipwa ada maalum na kuimarishiwa mazingira ya ufanyikazi.