Habari MsetoKimataifa

Ilani yatolewa kwa Wakenya walioko Sudan Kusini

February 22nd, 2018 2 min read

Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Bi Monica Juma. Picha/ Maktaba

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI Jumatano  ilitoa ilani ya usafiri kwa Wakenya wanaoishi Sudan Kusini, hali inayoweza kusababisha mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Ilani hiyo iliyotolewa kupitia kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Biashara za Kimataifa, ililenga zaidi Wakenya wanaoishi katika maeneo ya Upper Nile nchini humo, hasa majimbo ya Bieh, Latjoor, Akobo, Jonglei, Liech Kaskazini na sehemu za majimbo ya Maiwut, Nile Mashariki, Boma na Yei River.

Hatua hii si ya kawaida ikizingatiwa kuwa Kenya na Sudan Kusini ni nchi jirani zilizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na pia Kenya ni miongoni mwa nchi zilizo katika mstari wa mbele kujaribu kupatanisha pande hasimu zinazozozana nchini humo.

Ilani hiyo ilitolewa siku moja baada ya marubani wawili waliokuwa wametekwa nyara na wanamgambo Sudan Kusini kurejea nchini baada ya kuzuiliwa kwa siku 42.

Marubani Frank Njoroge na Kennedy Shamalla, waliachiliwa huru baada ya wanamgambo wa chama pinzani cha Sudan People’s Liberation Army-In Opposition (SPLA-IO) kulipwa ridhaa ya Sh11 milioni. Kulingana na wanamgambo hao, ajali ya ndege iliyofanyika mpakani ilisababisha kifo cha mwanamke mmoja na ng’ombe 11.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Bi Monica Juma, alipowalaki marubani hao alisema: “Serikali ya Kenya inakashifu hatua ya kikatili ya SPLM-IO kwa tukio ambalo lilikuwa ni ajali kwani sote tunajua ajali haina kinga.”

Eneo la Upper Nile nchini Sudan Kusini huwa na utajiri mkubwa wa mafuta. Limekumbwa na vita kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa upinzani kwa muda mrefu.

Katika ilani yake, serikali ya Kenya ilitaka wananchi wake wanaoishi Sudan Kusini au wanaopanga kwenda nchini humo waondoke katika maeneo yenye vita hasa sehemu ambapo kumekuwa na vita kwa miezi sita iliyopita.

Mbali na hayo, Wakenya wote wanaoishi nchini humo walitakiwa kujisajili katika ubalozi wa Kenya ulio Juba au kupitia barua pepe kwa anwani [email protected].

Wizara hiyo pia ilitoa wito kwa wananchi wake wawe wakipiga ripoti mara moja kuhusu hali za dharura zinazowakumba kupitia barua pepe kwa [email protected] au nambari ya simu +25420494992.