Michezo

Ilivyo, Liverpool hawana mshindani katika EPL na taji la kipute cha msimu huu ni lao!

December 31st, 2018 3 min read

NA CHRIS ADUNGO

NUSU ya idadi za mechi katika kampeni za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) tayari zimepigwa.

Vita vya kutoachwa nje ya mduara wa nne-bora kileleni mwa jedwali vinazidi kupamba moto na kibarua cha kutoambulia nafasi tatu za mwisho mkiani kinazidi kuwa mtihani mgumu kwa Huddersfield, Fulham, Burnely, Cardiff na Southampton.

Je, Manchester City wataweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza baada ya miaka 10 kutetea kwa mafanikio ubingwa wa EPL?

Je, Liverpool watakomesha ukame wa miaka 29 wa taji la EPL kabatini mwao msimu huu? Au je, itakuwa ni zamu ya Tottenham Hotspur kutawazwa wafalme wa soka ya Uingereza kwa mara ya kwanza tangu 1961?

Japo Liverpool wanapigiwa upatu wa kutia kapuni ubingwa wa EPL muhula huu, nahisi kwamba vikosi vya pekee vyenye uwezo wa kuvuruga matumaini ya miamba hao ni Man-City na Tottenham.

Liverpool wamepania kuweka kando mikosi ya 2008-09 na 2013-14 ambapo waliongoza jedwali la EPL hadi Krismasi kabla ya kupitwa na kuambulia nafasi ya pili mwishowe.

Katika misimu minane kati ya 10 iliyopita, klabu iliyokuwa ikiongoza jedwali la EPL baada ya kupiga nusu ya michuano yote ya msimu, ilitwaa ubingwa.

Baada ya kutinga fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu jana na kuanza kampeni za msimu huu wa 2018-19 kwa matao ya juu, Liverpool ni mpinzani ambaye kwa sasa amedhihirisha kuwa ana uwezo mkubwa usiostahili kupuuzwa. Kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kwa sasa ni timu tofauti kabisa.

Viwango vya wachezaji wengi wa Liverpool vimeimarika kiasi kwamba uwepo wa Sadio Mane, Momahed Salah na Roberto Firmino kambini mwao kunawafanya kuwa miongoni mwa klabu zinazojivunia safu bora zaidi za uvamizi. Zaidi ya hayo, wanajivunia huduma za difenda Virgil van Dijk na nyani Alisson Becker ambao wanashikilia rekodi za kuwa beki na kipa ghali zaidi duniani kwa sasa.

Hadi kufikia mwisho wa msimu uliopita katika EPL, Liverpool na Manchester United ndizo timu za pekee ambazo ziliishinda Man-City ligini. Silaha kubwa ya Liverpool ni uwezo wao wa kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza kupitia kwa wachezaji wao wenye kasi sana na ambao hawahitaji kupata nafasi nyingi za wazi ili wafunge mabao.

Huu ndio upekee wa kikosi cha Klopp. Kwa namna moja au nyingine, Liverpool ni timu ambayo ubora wake utadhihirika kila inapocheza na mpinzani aliye na mazoea ya kumiliki mpira kwa muda mrefu na ambaye anacheza soka ya kushambulia sana kama mabingwa washikilizi wa taji la EPL, Man-City.

Mnamo 2013, Klopp aliwachochea Dortmund kutinga fainali ya UEFA baada ya kuwabandua Real Madrid kwenye nusu-fainali. Ingawa kulikuwapo na klabu nyingi zenye vikosi bora zaidi kuliko Dortmund wakati huo, mfumo na upekee wa mbinu za ukufunzi wa Klopp uliwatambisha wapambe hao wa soka ya Ujerumani.

Man-City na Liverpool kwa sasa ndizo timu zilizo na vikosi bora zaidi katika EPL. Hata hivyo, iwapo kuna timu iliyo na nafasi kubwa sana ya kusambaratisha kabisa ndoto za miamba hao, basi ni Tottenham Hotspur ya mkufunzi Mauircio Pochettino.

Baada ya kupiga nusu za mechi za msimu huu, Tottenham wanazidi kudhihirisha ubabe wao katika soka ya Uingereza. Jinsi mambo yalivyo, dalili zote zinaashiria kwamba Tottenham wana kila nafasi na uwezo wa kutinga tena mduara wa tatu-bora msimu huu au hata kuwapiga kumbo washindani wao wakuu ambao ni Liverpool na Man-City kirahisi.

Hadi walipowaalika Wolves uwanjani Wembley mwishoni mwa wiki jana, Tottenham ndicho kikosi cha pekee ambacho hakikuwa kimeambulia sare katika mechi yoyote ya EPL.

Hadi kufikia sasa, ninakiri kwamba hakuna kitu kizuri zaidi kuliko kuwa shabiki wa Liverpool ambao walijisuka vilivyo kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kampeni za EPL msimu huu kupulizwa.

Usajili uliofanywa na Klopp msimu huu uliashiria wazi ukubwa wa kiu aliyonayo ya kutia kibindoni ufalme wa EPL na taji la UEFA. Japo matumizi yake ya fedha yalishtumiwa na mahasimu wake wakuu katika EPL, naona kwamba Klopp alipania kujenga kikosi thabiti kitakachohimili mawimbi ya ushindani katika EPL na UEFA hasa kwa kujinasia pia huduma za Naby Keita, Fabinho na Xherdan Shaqiri.