Michezo

Iliyotabiriwa yatimia: Mbappe afuata mastaa wenzake huko Real Madrid

June 3rd, 2024 2 min read

MADRID, UHISPANIA

MSHINDI wa Kombe la Dunia na Ufaransa mwaka 2018 mshambulizi Kylian Mbappe, amejiunga na Real Madrid ya Laliga kama mchezaji huru kutoka Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa.

Mkataba wake na PSG utarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu huku akiwa amefungia timu hiyo mabao 256 tangu alipojiunga nao kutoka Monaco kwa mkopo wa awali mwaka 2017.

Mamake, Fayza Lamari, amekiri kwamba ataenda “ambako kila mtu anajua” – lakini hakujakuwa na tangazo rasmi ya anakokwenda.

Hata hivyo, Madrid wanataka kusubiri hadi msimu wao umalizike kabla ya kutoa taarifa kwa umma.

Huku wakiwa na taji la 15 la Ligi ya Mabingwa Ulaya na kocha wa Ufaransa Didier Deschamps akisema alitaka mustakabali wa nahodha wake utatuliwe kabla ya Euro 2024, hatimaye Madrid wako katika nafasi ya kutangaza hilo.

Hawatarajii kumtangaza Mbappé rasmi hadi katikati ya Julai kwa sababu Ufaransa inajiandaa kwa mashindano ya Ubingwa wa Uropa.

Inabakia kuonekana ikiwa Mbappé pia atashiriki Michezo ya Olimpiki huko Paris.

Tetesi zilisema kuwa, alitaka kuhamia Bernabeu mnamo Februari na kisha akatangaza Mei kuwa ataondoka PSG mwishoni mwa msimu.

Mbappe, 25, sasa atahamia Uhispania wakati dirisha la uhamisho la La Liga litakapofunguliwa mapema mwezi ujao

Madrid wanatarajiwa kutangaza mkataba huo wiki ijayo na wanaweza kumwasilisha rasmi mshambuliaji huyo Bernabeu kabla ya Euro 2024.

Mbappe, amekubali mkataba na Real hadi 2029, akipata Sh2.1 bilioni (Pauni 15 millioni) kwa msimu, pamoja na bonasi ya kusaini ya Sh21.1 billioni (Pauni 128 millioni) kwa miaka mitano.

Mfaransa huyo atapata nafasi ya kucheza pamoja na Luka Modric, huku kiungo huyo wa kati wa Croatia akitarajiwa kusaini mkataba mpya wa kuitumikia klabu hiyo kwa mwaka mmoja.

Modric, 38, aliingia kama nguvu mpya kuchukua nafasi ya Toni Kroos kwenye mechi dhidi ya Borussia Dortmund Uwanjani Wembley Jumamosi, ambapo Madrid ilishinda 2-0 na kutwaa taji lao la 15 la Kombe la Mabingwa Ulaya.

Hiyo ilikuwa ni mechi ya mwisho ya Mjerumani Kroos, 34, kucheza baada ya kuitumikia timu hiyo kwa miaka 10.

Modric ambaye ni kiungo wa zamani wa Tottenham, mkataba wake unamalizika baadaye mwezi huu, lakini anatarajiwa kusalia kwa miezi 12 zaidi.