Habari Mseto

Imam aoa mwanamume akidhani ni mwanamke

January 13th, 2020 3 min read

Na DAILY MONITOR

MHUBIRI wa Kiiislamu nchini Uganda aliyeoa mwanamume akidhani ni mwanamke amesimamishwa kazi.

Sheikh Mohammed Mutumba wa msikiti wa Kyampisi Masjid Noor katika wilaya ya Kayunga, amesimamishwa kazi uchunguzi ukiendelea kuhusu alivyofikia hatua ya kuoa mwanamume.

Kadhi wa kanda hiyo, Sheikh Abdul Noor Kakande alisema Sheikh Mutumba, aliye na miaka 27, anachunguzwa kuhusiana na kisa hicho kisicho cha kawaida.

Naye Imam mkuu wa Kyampisi Masjid Noor, Sheikh Isa Busuulwa alisema hatua ya kumsimamisha kazi ni kwa lengo la kudumisha heshima ya dini.

Sheikh Busuulwa alikiri kuwa alihudhuria harusi hiyo katika mji wa Kyampisi, lakini akasema uongozi wa msikiti huo haukushirikishwa kwenye mipango ya posa na harusi.

Sheikh Mutumba alifanya harusi ya Kiislamu, Nikah (nikahi kwa Kiswahili), na Richard Tumushabe, ambaye alikuwa amejibandika jina la mwanamke la Bi Swabullah Nabukeera wiki mbili zilizopita.

Habari zinasema baada ya ‘kufunga ndoa’, wawili hao waliishi pamoja kama mume na mke kwa siku kadhaa. Lakini katika muda huo hawakushiriki tendo la ndoa kwa sababu ‘Bi Harusi’ alidai kuwa katika siku zake za hedhi.

Lakini kitumbua cha Tumushabe kiliingia mchanga wakati jirani yao mtaani alipodai kuwa ‘Bi Harusi’ aliruka ua unaotenganisha nyumba zao na kuiba televisheni na nguo zake.

Jirani huyo alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kayunga, ambapo baadaye Tumushabe alikamatwa na kupelekwa kituoni.

Afisa wa upelelezi katika wilaya ya Kayunga, Bw Isaac Mugera alisema Tumushabe alipofikishwa katika kituo cha polisi alikuwa amevaa hijabu na viatu vya wanawake.

“Kama kawaida ya utaratibu wa polisi, afisa wa kike alimkagua kabla ya kumtupa seli. Afisa huyo alishtuka kugundua kuwa alikuwa ameweka nguo kifuani ili ionekane kuwa ana matiti.

“Hii ilimfanya afisa kufanya ukaguzi wa kina ndipo akagundua kuwa Tumushabe alikuwa na sehemu za siri za kiume. Mara moja tulimjulisha ‘mumewe’ ambaye pia alikuwa hapo kituoni,” akasema Bw Mugera.

Habari hizo zilimshtua Sheikh Mutumba, ambaye aliwaomba polisi wamruhusu ajionee mwenyewe ndipo aweze kuamini.

Kuona ‘mkewe’ ni mwanamume, polisi walisema Sheikh Mutumba alipiga nduru kwa kutoamini tukio hilo.

Bw Mugera alisema walipomhoji mshukiwa alisema jina lake halisi ni Richard Tumushabe wa umri wa miaka 27, na kuwa alijifanya mwanamke ili kumhadaa Imaam kwa ajili ya kupata pesa kutoka kwake.

Akisimulia jinsi alivyojipata katika sakata hiyo, Sheikh Mutumba alisema alikutana na Tumushabe hapo msikitini wakati wa sala.

“Nilikuwa nikitafuta mwanamke wa kuoa na nilipoona msichana mrembo aliyevaa hijabu nilimwomba tuwe wapenzi na akakubali. Tulianza kuchumbiana lakini akaniambia hatutashiriki tendo la ndoa hadi nipeleke mahari kwa wazazi wake na pia tufunge ndoa ya Kiislamu,” akasimulia Imaam.

Aliongeza kuwa wiki moja baada ya kufahamiana, alimtembelea shangaziye Tumushabe, Bi Nuuru Nabukeera katika kijiji cha Kituula na akalipa mahari.

Bi Nabukeera, ambaye pia amekamatwa na polisi, alisema Sheikh Mutumba alipeleka mahari ya mbuzi wawili, magunia mawili ya sukari, katoni moja ya chumvi na Kurani.

Alijitetea kuwa hakuwa na habari kuwa Tumushabe ni mwanamume kwani walikutana akiwa mkubwa wakati huo akijifanya mwanamke.

“Siku ya kwanza aliponitembelea, alikuwa amevaaa hijabu na hata tulilala naye chumba kimoja. Aliponiambia amepata mchumba nilimshauri amlete nyumbani,” akaeleza Bi Nabukeera.

Mwadhini wa msikiti huo, Amisi Kibunga alisema alimwona Tumushabe mara mbili wakati wa sala kabla ‘hajaolewa’ na ilikuwa vigumu kujua kama ni mwanamume.

“Alikuwa na sauti nyororo na alitembea kama mwanamke. Pia kila wakati alikuwa anavaa hijab.”

“Siku chache baada ya harusi, Sheikh Mutumba aliniambia ‘mkewe’ amekataa kuvua nguo ili washiriki mapenzi. Nilikuwa nikipanga kwenda kumshauri nilipopata habari amekamatwa na polisi kwa madai ya wizi,” akasema Bw Kibunga. Majirani waliambia wanahabari kuwa Sheikh Mutumba hajaonekana kwa siku kadhaa tangu kisa hicho.

Jirani yake, Henry Mukwaya alisema Tumushabe, baada ya ‘kuolewa’ alikuwa akifanya kazi za kike kama kufua nguo, kuosha nyumba na kupika lakini mara nyingi alikaa ndani ya nyumba.

“Faili ya kesi imepelekwa kwa afisi ya Mkuu wa Sheria hapa wilayani ili tupate ushauri kabla ya kumshtaki mshukiwa. Tutamshtaki kwa makosa ya kujifanya mwanamke na wizi,” akasema Bw Mugera.

Bw Mugera aliwashauri vijana kutafuta mbinu za kisheria za kupata riziki badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya kijinga.