Imara United yalenga kupandishwa daraja muhula ujao

Imara United yalenga kupandishwa daraja muhula ujao

Na JOHN KIMWERE

IMARA United ni kati ya klabu kongwe nchini kama AFC Leopards maarufu Ingwe na Gor Mahia kwa jina lingine K’Ogalo ambazo hushiriki ngarambe ya Ligi Kuu ya Betking Kenya Premier League (BKPL).

Imara United awali ikifahamika kama Maragoli United ni kati ya timu zinazoshiriki mechi za Ligi ya Kaunti chini ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Tawi la Nairobi Magharibi.”Sina shaka kutaja kuwa ina wachezaji wazuri wanaolenga kufanya kweli na kutwaa tiketi ya kufuzu kushiriki mechi za Nairobi West Regional League (NWRL) muhula ujao,” alisema kocha wake, Milton Ombote na kuongeza kuwasoka la humu nchini linazidi kuimarika kila kuchao.

Kocha huyo anasisitiza kuwa klabu nyingi nchini hupitia wakati mgumu hasa ukosefu wa ufadhili hali ambayo huchangia wachezaji wengi kutopata nafasi kupalilia vipaji vyao.

Miaka saba

Klabu hiyo yenye makazi katika mtaa wa Huruma Kaunti ya Nairobi ni kati ya vikosi vinavyoshiriki mechi za Ligi ya Kaunti ya Nairobi msimu huu. Kadhalika kocha huyo anasisitiza kuwa endapo watafanikiwa kupata ufadhili na kuendelea kushiriki mechi za ligi miaka saba inatosha kufaulu kutinga kipute cha haiba kubwa nchini (Ligi Kuu).

”Kwa jinsi tunavyozidi kujituma kwenye kampeni za msimu huu hatuna mpinzani wa kututia kiwewe tumekaa vizuri kupambana mwanzo mwisho na kuandikisha matokeo mazuri,” alisema naibu wake, Ronado Mavuko na kuwataka wenzake kushiriki kila mechi kama fainali.

Picha/JOHN KIMWERE

Meneja wa klabu hiyo, Adeya Nerbard anatoa wito hasa kwa jamii ya Maragoli ijitokeze kufadhili wachezaji hao kwenye juhudi za kunoa wachezaji wanaokuja.Matatizo ya udhamini ndio yamechangia klabu hii kujikuta njia panda hasa kuvunjika na kufufuka mara ikivunjika na kufufuka.

Licha ya kupitia changamoto kibao za kifedha klabu hiyo inajivunia kukuza wachezaji wawili wa hivi karibuni Charles Owino na Victor Otieno waliobahatika kusakatia Gor Mahia na Sony Sugar mtawalia.

Mataji

Kwenye juhudi za kukuza talanta za wachezaji wake klabu hiyo imebahatika kubeba mataji kadhaa ikiwamo Chapa Dimba na Safaricom pia Super and Extreme Cup.

Imara inajumuisha:Ronado Mavuko, Felix Oyange, Maurice Omondi, Erick Owino, Edwin Campbell, Robert Ouko, George Odede, Kennedy Odour, Kevin Shikwa, Victor Otieno na Brian Omondi.

Wengine wakiwa Basil Owino, Mike Kosambo, Alex Murithi, Julius Mwangi, Brian Kioko, Joseph Milondo, Jacob Omondi, Charles Ochieng, Brian Odera, Calvince Ouma, Alfred Oyindi, Alli Tatai, Kenneth Omondi, Victor Odhiambo, Abdullai Abdi, James Moses na Emmanuel Odede.

Picha/JOHN KIMWERE
Timu ya soka ya Imara United
  • Tags

You can share this post!

Aliyejaribu kumuua Kosewe asema alikuwa akijikinga

Serikali yanyenyekea kuhusu amri kwa makanisa